Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe Ayoub Mohamed Mahmoud amesema utashi wa viongozi wa kitaifa wa kuhakikisha watanzania wanapata msaada wa kisheria umeifanya Tanzania kusifika Duniani kwa kujali watu wake.
Mhe. Mahmoud ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Kusini Unguja leo tarehe 10 Mei 2025 katika uwanja wa Azimio Mtende ambapo mgeni rasmi alikua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.
Amesema, Kampeni hii itawasaidia wananchi kufikiwa na huduma za Msaada wa kisheria kwa ukaribu bila gharama zozote ambapo watapatiwa huduma za ushauri wa masuala ya kisheria, uandishi wa nyaraka za kisheria, utatuzi wa migogoro pamoja na elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria.
Mhe. Mahmoud ameongeza kuwa Mtende iko kusini kabisa mwa mkoa wa Kusini Unguja na hivyo kufikisha huduma za Msaada wa kisheria katika maeneo hayo ni fursa kubwa kwa wananchi kutatuliwa migogoro yao.
Aidha amemuombea Rais wa Zanzibar kuwajengea shule ya msingi na sekondari ya ghorofa pamoja na kujenga barabara za lami za ndani Mtende.