Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inawatangazia wananchi na wateja wake kuhusu ofa maalum ya msamaha wa faini ya kurejeshewa huduma (reconnection fee) kwa wateja waliokatiwa maji kutokana na madeni ya bili.
Ofa hiyo imetolewa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maji, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji safi kwa urahisi zaidi.
Kupitia ofa hiyo, wateja wote wa DAWASA waliositishiwa huduma kutokana na madeni wanatakiwa kufika katika ofisi za Mamlaka zilizo karibu nao ili kuingia mkataba wa ulipaji wa madeni. Baada ya mkataba, huduma itarejeshwa bila kutozwa faini ya kawaida ya Shilingi 15,000.
DAWASA inawahimiza wateja wake kuchangamkia fursa hii adhimu, ambayo itakuwa wazi kuanzia tarehe 9 Mei hadi 31 Mei 2025.