Wakati huu Tanzania ikitarajiwa kuungana na nchi nyingine kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani, Mei Mosi, 2025 kwenye viwanja vya Liti Singida, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake, imetajwa kuwa na mafanikio makubwa katika kuujenga utumishi wa umma wenye tija na wenye kuzingatia masharti ya kazi na ustawi wa wafanyakazi wa kada zote nchini Tanzania.
Ndani ya Miaka hiyo minne ya Uongozi wake, Rais Samia amepunguza kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 9% hadi asilimia 8%, kufuta tozo (retention fee) ya asilimia 6 iliyokuwa inatozwa kutoka katika mishahara ya watumishi wa umma walionufaika na Mikopo ya elimu ya Juu, kulipa malimbikizo ya mishahara pamoja na kupandisha vyeo watumishi mbalimbali, suala ambalo halikuwa limefanyika kwa kipindi kirefu.
Kwa mwaka 2022/23 serikali ya awamu ya sita ilipandisha pia Kima cha chini cha Mshahara kwa asilimia 23.3% kutoka Shilingi 300,000 hadi shilingi 370,000 kwa mwezi, huku pia makundi mengine ya watumishi yakiguswa na mabadiliko hayo kwa viwango tofauti kwa kuzingatia ukomo wa Bajeti za serikali lengo likiwa ni kuwafanya watumishi wa umma kumudu gharama za Maisha.
"Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2025 madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 148,137 yenye jumla ya Shilingi 248, 528,998,254.79 yalipokelewa na kushughulikiwa. Aidha, katika kipindi hicho, madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wastaafu takribani 10,022 kutoka kwa waajiri yenye jumla ya Shilingi 33,290,109,780.75 yamepokelewa na kushughulikiwa na wahusika wamelipwa stahiki zao mbalimbali kupitia kwa waajiri wao.
"Kadhalika mpaka kufikia Machi, 31, 2025 Jumla ya watumishi wa umma 610,733 wamepandishwa vyeo, 42,515 wamebadilishwa kada, 3,208 wamepata uteuzi, 157,512 wamesafishiwa taarifa zao za kiutumishi, 10,725 wamebadilishiwa vyeo, 3,877 wamerekebishiwa majina, 9,269 wamefanyiwa mabadiliko ya mshahara binafsi, 2,558 wamerejeshwa kwenye utumishi wa umma na 133,317 wameajiriwa katika Taasisi mbalimbali za umma.
Aidha, katika kipindi hicho, Jumla ya nafasi za ajira 155,008 zimetolewa na jumla vibali vya ajira mbadala 41,673 vimetolewa ili kujaza nafasi zilizobaki wazi kwa sababu mbalimbali." Imekaririwa taarifa ya Ofisi ya Rais Menejiment ya utumishi wa Umma na Utawala bora Tanzania.
Katika hatua nyingine, serikali ya Rais Samia pia imefanya maboresho kwenye maslahi ya watumishi wa Umma kwa kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara (Annual Salary Increment) ambapo mwaka 2023/24 Shilingi 153, 926,496,703.68 kililipwa na kwa mwaka 2024/25 Jumla ya shilingi 150, 873,245,100 zilitengwa kwaajili ya nyongeza hiyo ya mwaka ya mshahara.