Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi Imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi Bilioni tano kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Taifa ya Akili Mirembe na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ili kuboresha Huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili, Dkt. Paul Lawala wakati akieleza mafanikio ya Miaka minne ya Rais Samia akiwa Madarakani.
Dkt. Lawala amesema kuwa fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya Jengo la wagonjwa wa Dharura, jengo la wagonjwa mahututi,ununuzi wa vifaa tiba na vitendanishi, jengo la vyumba 20 vya madaktari, nyumba mbili za kisasa za watumishi, ukarabati wa wa majengo ya 21 yaliyokuwa yamechaka na ujenzi wa uzio maeneo ya hospitali.
“Chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hospitali yetu inaendelea na miradi miwili muhimu ambayo ni ujenzi wa jengo la maabara ya kisasa na ujenzi wa Kituo cha matibabu ya uraibu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia na kudhibiti Dawa za Kulevya(DCEA) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu”, ameeleza Dkt. Lawala
Vile vile ameongeza kuwa Hospitali inatarajia kukamilisha miradi mbali mbali ya muhimu ikiwemo ujenzi wa Kituo cha ubora cha masuala ya afya ya akili (National Center of Excellence for Mental Health)
Aidha katika kipindi cha Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hospitali imeongezewa watumishi waliopo katika ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi wa matibabu ya afya ya akili.
“Mwaka 2020 Hospitali ilikuwa na madaktari bingwa wa tatu lakini mpaka kufikia sasa tunajumla ya madaktari bingwa 15 kati yao mabingwa wa afya ya akili tisa na sita wa kada nyingine”, amesema Dkt. Lawala
Pia amesema kuwa madaktari wengine saba wapo karibu kumalizia masomo ya ubingwa chini ya ufadhili wa Samia Schoral ship kupitia Wizara ya Afya.
Lakini pia amesema kuwa Hospitali inahudumia wastani wa wagonjwa 50,000 kwa mwaka ambapo kwa Huduma za wagonjwa wan je na wagonjwa wa ndani ni asilimia 60 na asilimia 40 ni wagonjwa wa magonjwa ya mwili.