Serikali ya Tanzania imebainisha mikakati madhubuti ya kuboresha upatikanaji wa dhahabu ghafi kwa ajili ya kiwanda cha Geita Gold Refinery (GGR), ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi kwa ufanisi. Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alieleza kuwa ili GGR ifanye kazi vizuri, inahitaji upatikanaji wa dhahabu ya kutosha (feed stock), na Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali kuhakikisha hilo linatokea.
Akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye semina iliyoandaliwa Februari 11, 2025, Mhe. Mavunde alifafanua kuwa Serikali tayari imefanya kikao cha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na wadau wengine ili kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa mitaji kupitia mpango wa Export Credit Guarantee Scheme, unaowafaidi Watanzania.
Waziri Mavunde alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wachimbaji wadogo wa dhahabu kuuza madini yao katika viwanda vya ndani, kama GGR. Lengo ni kuwafaidi kwa kupata bei nzuri na kupunguza gharama za usafirishaji, sambamba na faida ya punguzo la tozo zinazotozwa kwa dhahabu inayosafishwa nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alieleza dhamira ya Serikali ya kuongeza thamani ya madini nchini, ambapo alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza mapato ya Serikali, kutoa ajira, na kuboresha sekta nyingine zinazohusiana na madini kama vile viwanda na benki.
GGR, ambayo ni kiwanda cha kisasa cha kusafisha madini ya dhahabu, imeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini, huku Serikali ikijivunia uwepo wake kama chachu ya kuleta maendeleo. "Tanzania sasa ina miundombinu ya kisasa kwa usafishaji wa dhahabu, jambo linalokuza hadhi yetu duniani katika soko la madini," alisema Mavunde.
Vilevile, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, alisisitiza umuhimu wa viwanda vya ndani kufanya utafiti wa masoko ili kupambana na ushindani wa kibiashara, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, akielezea juhudi za Serikali kupunguza tozo za dhahabu inayosafishwa, jambo ambalo litahamasisha wachimbaji wadogo kuuza madini yao katika viwanda vya ndani.
Kamati ya Bunge pia ililipongeza kiwanda cha GGR na kuwataka wawekezaji kuendelea kuwekeza katika sekta ya madini, akiwemo Bi. Mwanahamisi Masasi, maarufu kama Mama Masasi, ambaye ameonyesha uthubutu mkubwa katika kuanzisha kiwanda hicho. Dkt. Mathayo David, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, aliitaka Serikali kuhamasisha uwekezaji zaidi katika madini ili kuongeza manufaa kwa uchumi wa taifa.