Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe leo Januari 25, 2025 ameongoza timu ya ya Wataalam pamoja na Wadau wa Sekta ya Afya kutembelea na kuona shughuli zinazofanywa katika Maabara tembezi ya Afya ya Jamii iliyopo katika Kituo cha Afya Kabyaile, Wilaya ya Misenyi Mkoa wa Kagera.
Dkt. Magembe amepongeza Wataalam waliopo katika Kituo hicho kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuchunguza sampuli mbalimbali za magonjwa hatarishi ikiwemo yale ya mlipuko.
Amesema kuwa ushirikiano zaidi baina ya Serikali pamoja na wadau unahitajika zaidi katika maabara tembezi nchini ili wataalam hao waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa sahihi za kimaabara kuhusu magonjwa mbalimbali.
Maabara hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika uchunguzi wa sampuli mbalimbali za magonjwa ya mlipuko ambapo imefanya kazi kwa ufanisi kuchunguza sampuli za ugonjwa wa Marburg uliotokea mwaka 2023 pamoja na 2025.