Mbunge wa Jimbo la Tanga Mhe Ummy Mwalimu tarehe 05/10/2024 amefanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Central ambapo yeye pamoja na diwani wa kata hiyo Mhe. Said Mbarouk (Ami Said) walielezea Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025 katika Kata ya Central na Jimbo la Tanga Mjini kwa ujumla.
Mhe Ummy na Mhe Saidi Mbarouk walieleza kuwa chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Ilani ya CCM imetekelezwa kwa mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji na umeme ambapo kwa kata ya Central kumefanyika ujenzi wa madarasa na ukarabati mkubwa wa Majengo katika Shule ya Sekondari ya Old Tanga uliogharimu shilingi milioni 450, Ujenzi wa eneo la forodhani yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6; na ujenzi wa barabara ikiwemo barabara ya Ocean View pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika mitaa mbalimbali ya Kata hiyo.
Akiongea katika mkutano huo, Mhe Ummy aliwahimiza wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo ya vikundi ya asilimia kumi kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3 kimetengwa.
Aidha Mhe Ummy na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe Abdarahman Shilloo wamewataka wananchi wa Jiji la Tanga kujiandikisha kwenye daftari la Mkaazi tarehe 11 hadi 20 mwezi Octoba 2024 na pia kushiriki kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024 na kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM na hiyo ndio itakuwa shukurani kwa Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa aliyowafanyia watu wa Tanga hasa suala la upanuzi wa bandari ya Tanga ambayo sasa meli kubwa zimeanza kutia nanga na kuongeza fursa za ajira na biashara kwa wakazi wa Tanga.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya ya Tanga wakiongozwa Ndg. Bashiru Mwasola, waheshimiwa madiwani wa Jiji la Tanga wakiongozwa na Mstahiki Meya Mhe Abdulrahman Shilloo, viongozi mbalimbali na wananchi wa kata ya Central na kata za jirani.