TUKIO LA KUTISHA LA UKATILI DHIDI YA MTOTO WA MIEZI SITA DODOMA


Taasisi ya Doris Mollel, tunasikitika kwa kutokea kwa tukio hili la kikatili ambalo linakiuka haki za msingi za mtoto na kuhatarisha mustakabali wa ustawi wa watoto nchini. Hivyo, tunatoa pole kwa familia ya mtoto wa miezi sita aliyeuawa kikatili baada ya kubakwa na baba yake mzazi katika eneo la Mbuyuni, Kata ya Kizota, jijini Dodoma.

Matukio haya ya kikatili yamekuwa yakijirudia nchini hivi karibuni, hivyo, tunalaani vikali vitendo hivi vya kinyama na vya kukosa utu. Ukatili dhidi ya watoto, na hususani ukatili wa kingono, ni uhalifu wa kusikitisha unaovunja haki za kibinadamu na kuathiri vibaya maisha ya watoto, familia zao, na jamii kwa ujumla. Tunahitaji kuchukua hatua za haraka kuzuia matukio ya aina hii yasijirudie. Tunatoa wito kwa serikali kupitia Jeshi la Polisi Tanzania, Kuharakisha uchunguzi na kuhakikisha kwamba baba huyu anachukuliwa hatua kali za kisheria kama mfano ili kuzuia matukio kama haya yasitokee tena.

Taasisi ya Doris Mollel tutaendelea kufuatilia matukio haya kwa ukaribu na kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mahakama, kuhakikisha haki inatendeka. Tunasisitiza kwamba watoto wote wana haki ya kuishi kwa heshima, usalama, na utu. Tunaomba jamii nzima kushirikiana na serikali na vyombo vya usalama katika kupambana na ukatili wa aina hii.

Post a Comment

Previous Post Next Post