WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekabidhi Hati za Hakimiliki za Kielektroniki kwa wananchi waliohamia Msomera kwa hiari wakitokea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na wale waliokuepo katika kijiji hicho kabla.
Akikabidhi Hati za Hakimiliki kwa wananchi hao wa Kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amewasisitiza kutoyauza maeneo yao na badala yake wayatunze kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Waziri Ndejembi amesema Serikali inatekeleza mradi wa kujenga nyumba na kuwapatia mashamba wananchi wanaohama kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda vijiji vya Msomera, Lengusero, Saunyi na Kitwai ‘B’ vilivyopo katika mkoa wa Tanga na kusisitiza maeneo yote yapangwe na kupimwa kwa ajili ya makazi na mashamba.
“ Nimesikia changamoto hapa kuhusu upangaji wa Msomera Center, kwamba kwingine pamepangwa vizuri ila pale palipokua kijiji hapajawekewa matumizi bora ya ardhi. Sasa ninamuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi kuhakikisha kwamba Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani pamoja na Mtendaji wa Tume ya Ardhi, sisi tunapoondoka wao wanabaki hapa ili kuhakikisha eneo lote la Msomera linapangwa,” Amesema Mhe Ndejembi.