WAGONJWA ZAIDI YA 70,000 WAFIKIWA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA


Kwa juhudi na weledi mkubwa, madaktari bingwa wa mpango wa "Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia" wamefanikiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya kwenye Hospitali 184 za ngazi ya Halmashauri nchini Tanzania. Zoezi hili limekuwa mkombozi kwa maelfu ya wagonjwa waliokuwa wakiteseka kwa magonjwa sugu, hasa uvimbe.

Akizungumza leo Agosti 7, 2024, katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alieleza jinsi mpango huu ulivyopunguza mateso ya wagonjwa na kuokoa maisha. "Tumeshuhudia mawe makubwa yakiondolewa kwenye vibofu vya mkojo, ikiwemo jiwe lenye uzito wa kilo 1 na gramu 200. Vilevile, watoto 20 wamefanyiwa upasuaji wa kurekebisha maumbile ya uume (hypospadias repair), hali ambayo ingewasababishia ulemavu wa kudumu," alisema Waziri Ummy.

Zaidi ya wagonjwa elfu 70 wamefikiwa kupitia mpango huu, huku huduma zikitolewa kwa asilimia tofauti kulingana na magonjwa. Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani waliona wagonjwa 22,057 (32%), magonjwa ya wanawake na uzazi 18,044 (26%), watoto 14,466 (21%), na madaktari bingwa wa upasuaji waliona wagonjwa 10,578 (15%). Kwa ujumla, wagonjwa 4,652 (7%) walipata huduma za upasuaji.

Mikoa kumi iliyoongoza kwa wagonjwa wengi waliojitokeza kupata huduma za madaktari bingwa ni pamoja na Tanga (4,410), Mara (3,671), Tabora (3,652), Mtwara (3,540), Mwanza (3,256), Ruvuma (3,253), Mbeya (3,126), Kagera (3,122), Pwani (2,966), na Manyara (2,964).

Kwa upande wa watoto, matatizo ya mfumo wa hewa na moyo yaliongoza kwa asilimia 16% (wagonjwa 2,352), ikifuatiwa na uambukizo kwa asilimia 15% (wagonjwa 2,091), upungufu wa damu au Sickle Cell kwa asilimia 9% (wagonjwa 1,287), na Nimonia kwa asilimia 7% (wagonjwa 1,030).

Mpango wa "Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia" umeonyesha jinsi juhudi za serikali zinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya. Hii ni hatua kubwa mbele katika kuboresha afya za wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote. Mapinduzi haya yanaonyesha umuhimu wa kuwekeza katika afya na elimu ya afya ili kuboresha maisha na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post