BASHUNGWA ASISITIZA ELIMU KWA WATOTO WA KIKE.


Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa wazazi na walezi kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha mtoto wa kike anaelimishwa ili kuleta matokeo chanya kwa jamii na Taifa.

Bashungwa ametoa wito huo leo Agosti 23, 2024 katika Sherehe za Mahafali ya sita (6) ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Mavuno na Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 30 ya Shirika la Mavuno yaliyofanyika Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

“Niwasihi Wazazi tuendelee kuhakikisha mtoto wa kike habaki nyuma, tuendelee kuungana na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwenye jambo hilo habaki nyuma anaendelea kulifanya kwa vitendo”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekamilisha ujenzi wa shule maalum za wasichana kila mkoa kwa ajili ya masomo ya Sayansi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Hatahivyo, Bashungwa amelipongeza Shirika la Mavuno kwa kuendelea kushirikiana na Serikali hususan Wilaya ya Karagwe na Kyerwa kwa kuwasaidia wananchi katika Sekta za kilimo, maji, elimu, nishati endelevu na mazingira.

Bashungwa amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mavuno, Charles Bahati kwa kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo katika vijiji 45 za Wilaya ya Karagwe na Kyerwa ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mawasiliano ya barabara ndani ya Mkoa wa Kagera na mikoa mingine ili kuwezesha Mkoa wa Kagera kufikika kiurahisi na kutokuwa kikwazo cha watoto kufika mashuleni kiurahisi.

Bashungwa amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuunganisha Wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Kagera kwa kiwango cha lami unaendelea pamoja na kuimarisha barabara ambazo zilikuwa hazipitiki hata kwa kiwango cha changarawe ili kurahisisha mawasiliano na shughuli za kilimo na biashara kutokwama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la MAVUNO, Charles Bahati ameeleza kuwa shirika hilo lisilokuwa la kiserikali (NGO) limewafikia wakulima 55,935, vikundi 1,865 vya vijana, akina mama na makundi mengine, vikundi 45 na kuwawezesha namna sahihi ya ufugaji nyuki pamoja na kuanzishwa kwa vitaru vya kuotesha miti 13,907 ngazi ya Kaya na vitalu 1,013 ngazi ya vikundi na taasisi ambapo Jumla ya miti 4,700,347 imepandwa ndani ya jamii.

Naye, Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe, Rasul Shandala ameeleza kuwa Shirika la Mavuno limeendelea kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Karagwe katika miradi mbalimbali ikiwemo ya Kilimo endelevu, Maji na Usafi wa mazingira, Elimu na Nishati endelevu na kuahidi kuendeleza mashirikiano hayo kwa ajili ya kuhudumia jamii inayowazunguka.

Post a Comment

Previous Post Next Post