Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema sekta ya utalii nchini Tanzania inaendelea kufanya vyema ikichangiwa pia na utunzaji wa malikale na maeneo mengine ya urithi wa Dunia.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo katika mahojiano aliyoyafanya pembeni mwa Mkutano wa 46 wa Kamati ya Maeneo ya Urithi wa Dunia chini ya Unesco unaoendelea jijini hapa ambapo miongoni mwa taarifa za uhifadhi (state of conservation reports) zitakazowasilishwa zipo zitakazogusa maeneo yaliyolindwa kama sehemu ya urithi wa dunia kama Serengeti, Ngorongoro, Nyerere/Selous na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
“Maeneo haya yamekuwa na mchango mkubwa sana kukuza utalii kwa sababu yamekuwa moja ya vivutio tunavyovitegemea na tuko hapa kuonesha mshikamano na dunia nzima katika kuendelea kuweka nguvu za pamoja kuyahidadhi na kuyatangaza,” alisema Dkt. Abbasi akigusia kuwa takwimu za miezi sita (Januari-Juni, 2024) zinaonesha utalii umeongezeka kwa takribani asilimia 25 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023.
Mkutano huo pia unahudhuriwa na Waziri wa Utalii na Mambokale wa Zanzibar Mhe. Mudrik Soraga na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambaye pia ni Mwakilishi wa Tanzania katika Unesco, Balozi Ali Mwadini.