BASHUNGWA AKEMEA TABIA YA VIONGOZI KATIKA KATA KUCHONGANISHANA.


Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amekemea tabia ya viongozi wa kisiasa katika kata ya Kituntu Wilayani Karagwe kuvutana na kuchonganishana na kupelekea kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi katika kata hiyo.


Ameeleza hayo Julai 05, 2024 katika mkutano wa hadhara  uliofanyika katika kijiji cha Katwe Wilayani Karagwe Mkoani Kagera na kuwataka viongozi hao kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili waweze kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayopelekwa na Serikali.


“Niwaeleze tu, changamoto katika kata ya Kituntu ni ya viongozi kutoshirikiana kwa pamoja na kuwepo kwa maneno ya uchonganishi baina yenu, badala ya kutumia muda huo kuwahudumia wananchi, hizo ni siasa za kizamani, achaneni nazo ili muweze kusukuma maendeleo kwa wananchi”, amesisitiza Bashungwa.


Bashungwa amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kuwainua wakulima wa zao la Kahawa na kuwezesha bei ya kahawa kuongezeka Kutoka bei iliyozoeleka ya 1,100 hadi kufikia 4,100 kwa kilo moja ya maganda ya Kahawa aina ya Arabika.


Bashungwa ameeleza mafanikio ya sekta ya Elimu katika  Kata ya Kituntu ambapo Shule ya Sekondari ya Kituntu inaendelea kuboreshwa na zaidi ya Shilingi Milioni 360 zimepelekwa kujenga miundombinu kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano.


Kuhusu miundombinu ya Barabara, Bashungwa ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imefanikiwa kufanya matengenezo ya barabara mbalimbali zinazounganisha Vijiji na Vijiji, Kata ya Kituntu na Kata jirani.


Aidha, Bashungwa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na amewahimiza kufuatilia kikamilifu fedha inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi na huduma kwa wananchi.


“Nikupongeze Mkurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara zote kushiriki katika mikutano hii ya wananchi pamoja na kusikiliza kero na kuyatolea majawabu na suluhu ya changamoto mbalimbali zinazokabili kata zote za Karagwe”, amesema Bashungwa. 


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karagwe, Paschal Rwamgata amesisitiza wananchi wa kata ya Kituntu kuhakikisha wanajitokeza na kujiandikisha kwenye maboresho ya daftari la Kudumu la wapiga kura muda utakapofika.


Naye, Diwani wa Kata ya Kituntu, Zidna Tayebwa amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kuendelea kuleta fedha na kusukuma miradi mingi ya maendeleo katika Kata hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post