DKT. MOLLEL AONYA VIKALI MAAFISA UTUMISHI KUINGILIA MAJUKUMU YA MAKATIBU WA AFYA


Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amewaasa  makatibu wa Afya nchini  kufanya kazi kwa kujiamini, Uadilifu na Ueledi kwa kuzingatia Miongozo na Kanuni na taratibu zilizopo ili kuepusha migongano na malalamiko katika taasisi walipo.

Dkt. Mollel ameitoa kauli hiyo Jijini Arusha wakati akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Makatibu wa Afya Nchini.

Dkt.  Mollel amesema Makatibu wa Afya ngazi zote za kutolea huduma za afya wameleta mafanikio na mabadiliko makubwa ndani ya sekta ya afya nchini.

"Hivi sasa idadi ya vyuo vinavyotoa mafunzo ya Kada ya Makatibu wa Afya imeongezeka ikiwa ni kielelezo cha umuhimu wa kada hiyo katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini" amesema Mollel. 

Wakati huo huo Dkt. Mollel ameilekeza Wizara ya afya kubainisha wazi majukumu ya Maafisa utumishi na Makatibu wa Afya kwenye  Hospitali za Rufaa za Mikoa ili kuzuia migongano katika utendaji.

"Jambo hili lichukuliwe kwa uzito na utatuzi wa haraka kwani kada zote hizi ni muhimu hivyo, misuguano yao inaleta madhara makubwa kwa watumishi na wagonjwa wanaoenda kupata huduma kwenye taasisi hizi,"amesema Dkt.Mollel.

Dkt.Mollel amesema Makatibu wa Afya  ndio wasimamizi wa rasimali na nyenzo za kutolea huduma za afya hivyo wanatakiwa kufanya  maandalizi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya Bima ya Afya kwa Wote ili utekelezaji ukianza ulete matokeo bora.

Post a Comment

Previous Post Next Post