Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Ndg. Mohammed Ali KAWAIDA (MCC) ameuelezea Umma wa Watanzania kuwa wananchi wa Rufiji na Kibiti wanahitaji misaada ya kibinadamu na sio maneno matupu.
Ndg. Kawaida ameyasema hayo leo tatehe 11 Aprili, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Rufiji mkoani Pwani alipotembelea Kambi za waathirika wa mafuriko yanayoendelea katika Wilaya ya Rufiji na Kibiti mkoani Pwani kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu.
"Ndugu zangu wa Rufiji na Kibiti awali ya yote niwape pole sana kwa hichi kilichotokea, Rufiji hii si mara ya kwanza kukumbwa na hii kadhia ya mafuriko, historia inatueleza kuwa miaka kadhaa iliyopita maruriko yameshatokea kwa vipindi tofautitofauti."
"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu ikiwa ni pamoja na kujenga Bwawa kuwa la kuhifadhia maji ambayo yatatumika kwa kilimo cha Umwagiliaji"
"Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuona umuhimu wa kutoa misaada kwenu leo nimeambatana na Viongozi wenzangu Makamu Mwenyekiti UVCCM Ndg
Rehema Sombi (MNEC) na Katibu Mkuu UVCCM Ndg. Jokate Urban Mwegelo (MNEC) kuwaletea mahitaji muhimu yakibinadamu ikiwa ni pamoja na Mchele kilo 3200Kg na Mafuta ya kupikia lita 500" amesema Ndg. Kawaida
Aidha Ndg. Kawaida amewaomba Watanzania hususan wananchi wa Rufiji na Kibiti kupuuza maneno ya baadhi ya watu wanaopotosha Umma kwa maslahi yao binafsi kwa kuhusisha mafuriko haya na Ujenzi wa Bwawa la Mwl. Nyerere (JNHPP).
"Tunatambua kuwa kila mtu ana Haki ya Kikatiba ya kuzungumza na kutoa maoni, tunachoomba kwao wasipotoshe Umma kama hawawezi ni bora wakae kimya, Wananchi hawa wanahitaji Faraja na Misaada kipindi hichi na sio maneno"
Mwisho Ndg. Kawaida ametoa wito kwa Wanasiasa, Wafanyabiashara na watu mbalimbali kutoa misaada mbalimbali kwa wananchi wa Rufiji na Kibiti pamoja na kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Pwani na wakuu wa wilaya husika kuhakikisha misaada hii inawafikia walengwa na kugawanywa bila ya ubaguzi wowote
