MASHINE YA KUSUKUMA MAJI YAKOSESHA HUDUMA MWEZI MZIMA


Wananchi zaidi ya 5000 kutoka Vijiji vya Zanzui na Mlimani, kata ya Zagayu Wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu, wamekosa huduma ya maji safi na salama baada ya mashine ya kusukuma maji katika mradi wa maji uliopo kwenye vijiji hivyo kupata hitilafu ya Umeme.

Aidha, Mradi huo wa maji uliopo Zanzui umekuwa ukihudumia wananchi  katika vijiji hivyo, ulikuwa ukiwapatia maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Wakizungumza na waandishi wa Habari waliofika katika vijiji hivyo, wananchi hao walisema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja sasa, hawana huduma ya maji safi na salama kutokana na mashine iliyokuwa kwenye mradi huo kuungua.

Walisema kuwa tangu mashine hiyo (Moter) ipate hitilafu ya kuungua, wananchi hao hawapati maji ya bomba na kusababisha adha kubwa ya kupatikana kwa huduma hiyo muhimu katika jamii.

“Tunahangaika sana kupata maji kwa sasa, ni mwezi mmoja umepita hatupati maji ya bomba, tumerudi kwenye maji ya madimbwi, mito na majaruba ambayo siyo safi na salama, tunaomba serikali itutatulie changamoto hii,” alisema Pendo Matoke, mkazi Zanzui.

Awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Zanzui Michael Mabula alisema kuwa mradi huo, upo chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya, ambapo wamefika katika mamlaka hiyo lakini hawajapata ufumbuzi wa tatizo hilo.

“Kama viongozi wa hivi vijiji, tulifika hadi RUWASA ambao ndiyo wenye huu mradi, kufuatilia utatuzi wa changamoto hii, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika, kwa sasa wananchi tunatumia maji ya madimbwi yanatotumiwa na mifugo pia,”alisema Mabula.

Naye Meneja wa RUWASA Wilaya hiyo Mhandisi Hussein Yahaya alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, huku akibainisha kuwa chanzo cha tatizo hilo ni kuungua kwa mashine (Moter) ya kusukuma maji kwenye matenki.

“Ni kweli hilo tatizo lipo, na kama Mamlaka tumempata mzabuni wa kununua mashine hiyo na wiki hii tutakamilisha taratibu za manunuzi na kuifunga… tuwatoe hofu wananchi wa vijiji hivyo, wiki hii huduma ya maji itarejea,” alieleza Mhandisi Yahaya.

Post a Comment

Previous Post Next Post