JAMII YAKUMBUSHWA KUWAOMBEA NA KUWASAIDIA WATU WENYE MAHITAJI


Jamii imeaswa na kukumbushwa kuwasaidia watu wenye mahitaji na kuwajali kwasababu matendo hayo huwaweka karibu na Mwenyezi Mungu.

Hayo yamesemwa jana na Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Alhaj Mustafa Shaban Rajab wakati wa hafla ya futari kwa watoto yatima iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini katika Shule inayolea watoto yatima ya Zam Zam iliyopo Miyuji,Jijini Dodoma.

Sheikh Mustafa Rajab Shaban amempongeza Mbunge Mavunde kwa kuwajali watoto hao ambapo kila mwaka hushiriki nao futari na kuwagawia misaada mbalimbali jambo ambalo amesema ni mfano wa kuigwa na hivyo kuitaka jamii kuona umuhimu wa kuwasaidia wenye mahitaji.

“Tangu nikukutanishe na Mwanzilishi wa Kituo hichi Marehemu Sheikh Rashid Bura,umekuwa msaada mkubwa sana kwa hawa watoto na ni kama wanamuona Sheikh Bura bado yu pamoja nao.

Tutaendelea kukuombea kila siku kwa wema wako kwetu na jamii ya waislamu hapa Dodoma,unafanya mambo ya kumpendeza Mungu kwa kuwajali na kuwashika watu wenye mahitaji tendo ambalo ni ibada kubwa sana”Alisema Sheikh Mustafa

Akisoma risala kwa niaba ya watoto wenzake,Mtoto Fatuma Mohamed Ngogotaty amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwa msaada na kuwalea hapo shuleni kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ikiwemo vifaa vya michezo na vyakula na kuwasilisha ombi la kusaidiwa kujengewa msikiti na kumalizia uzio wa shule.

Akizungumza katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amesema kwamba mara baada ya kifo cha rafiki yake Sheikh Rashid Bura mwanzilishi wa Shule hii amejikuta na wajibu mkubwa kuendeleza huduma ambayo watoto hawa yatima walikuwa wanaipata na kwamba ataendelea kuyafanya haya kila wakati kwa watoto hao malaika vipenzi wa Mwenyezi Mungu.

Mh Mavunde pia alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia kwamba atatimiza maombi yao ikiwemo la kujenga msikiti na kumalizia uzio wa shule.

Hafla hiyo ya futari iliyohudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde Charles Mamba na Katibu Mwenezi CCM Wilaya Cde Aman Mulagizi  ilienda sambamba na dua kwa Taifa Tanzania na mahsusi kwa Mh Rais Dkt. Samia S . Hassan na viongozi wote.

Post a Comment

Previous Post Next Post