Serikali ya Awamu Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yatekeleza ombi la siku nyingi la wachimbaji wadogo Wilayani Songwe kwa kuwatengea eneo la uchimbaji na kuwakabidhi jumla ya leseni ndogo 37 zilizopo eneo la Kata ya Saza kutoka Leseni hodhi namba RL0009/2014 ya iliyokuwa Kampuni ya Bafex Tanzania Limited.
Hayo yameelezwa leo tarehe 23 Machi, 2024 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde alipofika eneo la Saza Wilayani Songwe kukabidhi leseni 19 kwa wachimbaji wadogo wa Kikundi cha Songwe Gold Family (SGF) na wachimbaji wengine wadogo wadogo 18 huku mchakato wa kuendelea kutoa Leseni zaidi ukiendelea.
"Nimefika hapa leo kwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amenielekeza nije kuwakabidhi leseni zenu za wachimbaji wadogo mlizomuomba na kuwa mnakwenda kuwekeza mitaji mikubwa sasa na kuongeza mzunguko wa fedha zitokanazo na shughuli za madini kufikia zaidi ya Trilioni moja.
Pamoja na kwamba mnachimba kwa kubahatisha, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari, 2024 mmezalisha kilo 729.6 zenye thamani ya bilioni 101.06, ninaamini kwa kupatiwa leseni hizi hamtakwenda kumwangusha Mhe. Rais kwa kuongeza uzalishaji na mapato yatokanayo na madini.
Pia, Mhe. Mavunde alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inaondoa ujanja ujanja kwenye shughuli za uchimbaji madini ambapo tayari ameshatangaza kufuta jumla ya leseni na maombi 2648 ambazo hazijaendelezwa na zimekiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini.
Mhe. Mavunde aliendelea kusisitiza kwamba hatasita kuendelea kufuta leseni kwa wamiliki wote ambao wanakiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini, ambapo alitoa mfano wa uwepo wa baadhi ya watu 6 tu wanaomiliki leseni zenye ukubwa wa zaidi ya ekari milioni 13.
Vilevile, Mheshimiwa Mavunde aliahidi kuwa baada ya Serikali kuwakabidhi wachimbaji wadogo Leseni ndogo za uchimbaji, inakwenda kuweka utaratibu mzuri wa kukabidhi taarifa za utafiti wa eneo hilo kwa kikundi cha SGF na pia kumuagiza Mkuu wa Wilaya kuhakikisha wachimbaji kwamba leseni tatu namba 10, 11 na 12 ziwe wazi ndani ya siku 14 ili kupisha maeneo hayo kutangazwa ili kupata uwekezaji mkubwa.
Awali, akisoma risala kwa Mhe. Mavunde, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wachimbaji wadogo cha Songwe Gold Family (SGF), Ndugu Simon Ndaki alibainisha kwamba Kikundi chao kiliomba siku nyingi maeneo ya kuchimba na kupelekea kushindwa kuwekeza mitaji mikubwa kutokana na kukosa uhakika wa maeneo. Tunaahidi sasa kwamba tunakwenda kuwekeza mitaji mikubwa na kuhakikisha tunaongeza mchango zaidi wa mapato ya halmashauri na Pato la Taifa kwa ujumla.
Akieleza kuhusu masuala mbalimbali ya Songwe, Mbunge wa Jimbo la Songwe, Mheshimiwa Philipo Mulugo aliishukuru Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu. Aliongeza kuwa Waziri Mavunde apeleke shukrani za wachimbaji wadogo kwa Rais wetu na kwamba wapo tayari kusaidia kurejesha fedha zaidi ya bilioni 72 zilizolipwa Bafex Tanzania Limited kwa uzalishaji mkubwa wa dhahabu.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mheshimiwa Solomon Itunda alieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya Wilaya yanatokana na shughuli za uchimbaji madini, na kuahidi kwamba ataendelea kushirikiana na wachimbaji wadogo kuhakikisha sekta ya madini inakua zaidi Wilayani Songwe.