Serikali kupitia Wizara ya Madini imepanga kutumia shilingi bilioni 35 kujenga jengo pacha la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha. Kujengwa kwa jengo hilo kunalenga kuongeza udahili kutoka wanafunzi 180 hadi 450 kwa mwaka.
Kaimu Mratibu wa kituo hicho, Mhandisi Ally Maganga, ametoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu mradi huo wa ujenzi.
Jengo hilo litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, makumbusho, masoko ya madini ya vito, karakana za uongezaji thamani madini, maabara za madini ya vito na bidhaa za usonara, pamoja na ofisi na mabweni ya wanafunzi.
Pia, litatumika kwa utoaji wa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito, minada ya madini ya vito na maonesho ya madini.Mhandisi Maganga amesisitiza kuwa jengo hilo litakuwa ni kitovu cha madini ya vito barani Afrika, ikizingatiwa wingi wa rasilimali madini ya vito nchini Tanzania.
Kuhusu miundombinu ya jengo hilo, ofisi za Tume ya Madini na biashara ya minada ya madini ya vito zitapatikana ndani yake, hivyo kuchangia katika kuleta fedha za kigeni nchini.Aidha, Mhandisi Maganga ameeleza kuwa TGC itakuwa mkombozi kwa wadau wa madini ya vito na metali katika kuchakata na uthaminishaji, kwani bado nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto kubwa ya teknolojia ya kusanifu madini.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili ijayo baada ya taratibu zote kukamilika.