BABYMOON NA DORIS MOLLEL FOUNDATION WAKABIDHI VIBEBEBEO VYA WATOTO WACHANGA 200


Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana na Kampuni ya Babymoon Care Products hapo jana walikabidhi vibebebeo vya watoto wachanga 200 katika hafla fupi iliyofanyika katika kumbi za mikutano ya Hoteli ya Dodoma, jijini Dodoma na kuhusisha Kamati za Bunge za Afya na Masuala ya Ukimwi pamoja na wawakilishi wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. 

Akifungua hafla hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel, alipongeza jitihada hizi bunifu za kuboresha utoaji huduma kwa watoto wachanga kupitia huduma ya ngozi kwa ngozi (Kangaroo Mother Care) pamoja na kuongeza nafasi za ajira kwa watanzania. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Mhe. Stanslaus Nyongo, aliwakaribisha wageni hao kutoka Uholanzi na kusema kuwa Kamati wamepokea wazo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano pale utakapohitajika. 

Kwa niaba ya Kampuni ya Babymoon, Dr. Hugo van der Zee, alishukuru kamati kwa kupokea wazo hili na kueleza kuwa wako katika mipango ya kutengeneza kiwanda cha vibebeo hivyo hapa Tanzania, na hivyo kuongeza nafasi za ajira kwa watanzania. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel, aliishukuru kamati kwa kuwa tayari kupokea mawazo mbalimbali na hasa bunifu yanayojikita katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa watoto wachanga hasa wanaozaliwa kabla ya wakati na kuahidi kuwa kama wadau wakubwa wa afya ya mama na mtoto nchini watazidi kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania wenye nia kuboresha utoaji huduma kwa watoto wachanga nchini. Pia, aliwakumbushia wajumbe wa kamati kuhusu maboresho ya likizo ya uzazi kwa akina mama wanaojifungua kabla ya wakati.

Post a Comment

Previous Post Next Post