Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde kuhakikisha wanafanya msawazo wa walimu katika shule zote zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo baada ya ziara yake ya kukagua mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam leo Januari 8 mwaka 2024.
Amesema kupitia utaratibu wa viongozi kupita shuleni kupokea wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wamebaini mlundikano wa walimu kwenye baadhi ya shule huku kukiwa na walimu wachache kwenye shule zingine.
“Sasa namuelekeza Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu OR-TAMISEMI kufanya msawazo wa walimu nchi nzima ili kuwe na uwiano sawa wa walimu na wanafunzi katika shule zote. Sio shule ina wanafunzi wachache lakini ina walimu wengi ili hali shule zingine zikiwa na walimu wachache na kuwa na wanafunzi wengi.”
“Kila mtanzania ana haki ya kupata elimu kutoka kwa walimu waliopangwa na Serikali hivyo mgawanyo stahiki ufanyike ili walimu waliolundilama kwenye shule za mjini wapelekwe kwenye shule za pembezoni ambazo nazo zina uhitaji mkubwa wa walimu.”
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema asubuhi ya leo ametembelea shule ya Sekondari Osterbay, Shule ya Msingi Muhimbili na Umoja wa Mataifa na kukuta zaidi ya nusu ya wanafunzo wamesharipoti kwa siku ya kwanza.
“Katika shule ya Sekondari Osterbay nimekuta ina wanafunzi takribani 1,000 lakini kuna walimu 20 tu ili hali katika shule hii ya Sekondari ya Benjamin Mkapa ina wanafunzi 1,600 na ina walimu 100.”
Mwaka 2024 idadi ya wanafunzi wanaotegemea kuandikishwa katika elimu ya awali ni 1,877,484 na mpaka Januari 5 mwaka huu wanafunzi walioandikishwa ni 918,205 sawa na asilimia 48.9.
Kwa upande wa darasa la kwanza wanafunzi walioandikishwa ni 1,191,627 sawa na asilimia 68.9 ya watoto 1,729,180 wenye umri wa miaka 7 wanaotarajiwa kusajiliwa.
Pia wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2024 ni 1,092,960.