Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi wa Maji uliojengwa eneo la Butimba Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza unaozalisha kiasi cha lita milioni 48 kwa siku.
Hayo yamedhihirishwa Januari 08, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Damian Sillo (Mb) wakati wa ziara ya kukagua hatua ya utekelezwaji wa mradi huo.
“Kamati imeridhishwa na mradi huu wa maji na tunatoa pongezi kwa Rais wetu Dkt. Samia Suliuhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani, tumejionea namna mradi huu ulivyotekelezwa umezingatia viwango vyote vya ubora,” amesema.
Mhe. Sillo amesisitiza kuwa Kamati haitokuwa kikwazo katika upatikanaji wa fedha ili miradi mingi itekelezwe na ikamilike kwa ubora na kwa wakati hasa ikizingatiwa kuwa jukumu lake la msingi ni kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi
Katika ziara hiyo, Kamati imeielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha inaendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa miradi ya maji kote nchini ili dhamira ya Rasi. Dkt. Samia Suluhu Hassan itimie kikamilifu.
“Tunaipongeza Wizara ya Maji, chini ya usimamizi wa Waziri wake Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kwa kuwa msitari wa mbele kuhakikisha dhamira ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani inatimia; Rai yetu ni kwamba Wizara ihakikishe hairudi nyuma na inapeleka miradi kwenye maeneo yote yenye changamoto,” ameelekeza Mhe. Sillo.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) alipokea maelekezo ya Kamati na ameihakikishia kuwa Wizara haitorudi nyuma kuhakikisha dhamira ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani inatimia
Mhe. Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo mkubwa wa Maji Jijini Mwanza ambao amesema umeanza kunufaisha baadhi ya maeneo.
Waziri Aweso ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaunganishwe na huduma ya maji na kusiwe na sababu zisizo za lazima katika kutimiza zoezi hilo.
Tags
Habari