WIZARA YA MADINI, WADAU WAJADILI IKOLOJIA MAENEO YA UCHIMBAJI


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali  leo Novemba 3, 2023 ameongoza taasisi  zinazofungamana katika shughuli  za uchimbaji sambamba na wawekezaji ili kujadili changamoto za ikolojia katika maeneo ya uchimbaji.

Hayo yamejiri katika kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilicholenga kupata uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa kila sekta zinazohusika katika usimamizi wa sheria katika shughuli  za uchimbaji madini

Akizungumza katika kikao hicho, katibu Mkuu amesema Serikali ipo makini kuhakikisha inatengeneza mazingira  wezeshi kwa wawekezaji na kuhakikisha  wanafanya uchimbaji  unaofuata sheria za nchi ili kuongeza pato la  Taifa na kuwanufaisha wananchi.

Katibu Mkuu Mahimbali  amewataka wataalamu katika sekta mbalimbali zinazohusika na kutoa vibali kwa wawekezaji wa madini kutekeleza majukumu  yao na kuharakisha  michakato ya upatikanaji wa Vibali hivyo ili kuruhusu shughuli  za uchimbaji kuendelea.

Aidha, wataalamu wamejadili kwa pamoja umuhimu  wa kufanyika kwa Tathimini ya Kimazingira  ya Kimkakati  (SEA) katika maeneo yote yanayohusisha miradi mingine zikiwemo shughuli za uchimbaji   ili kulinda ikolojia ya eneo husika.

Kikao  hicho cha pamoja  kimekwenda sambamba  na wasilisho la maendeleo  ya mradi kutoka kampuni ya MANTRA yenye  leseni ya Uchimbaji wa Madini  ya Uranium  katika mto Mkuji Wilayani Namtumbo mkoani  Ruvuma  na kuahidi kufuata sheria na matakwa ya Serikali  katika kuendeleza  mradi huo.

Kikao hicho kimehusisha wataalamu kutoka Wizara  ya Madini, Tume ya Madini, Taasisi ya Utafiti na Jiolojia, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Ardhi na Maendeleo  ya Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati TANAPA,  Mamlaka ya Wanyama Pori (TAWA), TAWIRI, NEMC  na TANESCO.

Post a Comment

Previous Post Next Post