TANZANIA NA ZANZIBAR ZAENDELEA KUDUMISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA UJENZI.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameahidi kuendelea kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Sekta ya Ujenzi kwa asilimia 100 ili maswala ya  uboreshaji wa miundombinu ya ujenzi yaweze kupatikana katika maeneo yote mawili ya bara na visiwani. 

Ameyasema hayo leo tarehe 11 Novemba 2023 Jijini Mwanza katika mkutano wa sita wa sekta hiyo uliobeba kauli mbiu ya "Mashirikiano Imara kwa Miundombinu na Muungano Imara" na kuahidi kusimamia kwa karibu mapendekezo na maazimio yote yanayokubaliana katika mikutano inayofanyika kwa faida ya pande zote mbili za Muungano. 

Aidha, Bashungwa amempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dr. Hussein Mwinyi kwa kutimiza miaka mitatu tangu aingie madarakani na kwamba katika kipindi hicho kumekuwa na mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Ujenzi ambayo ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa Sekta ya Utalii, Elimu na Afya na hivyo kukuza uchumi wa Taifa kiujumla. 

“Tumeona mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Utalii kupitia Royal Tour ambayo  alishirikiana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza fursa na vivutio vya nchi yetu bara na visiwani ambapo ukiangalia takwimu za wageni upande wa Zanzibar na Bara zimeongezeka kwa kweli lakini tunaona mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Miundombinu Zanzibar, kwenye Sekta ya huduma za jamii, Elimu na Afya hivyo ni lazima tuwapongeze viongozi wetu hawa”, amesema Bashungwa 

Ameongeza kuwa mbali na utaratibu wa kukutana Sekta ya Ujenzi imechukua fursa ya mkutano huo na kukubaliana pande zote mbili kusaini mkataba wa makubaliano ambao watakuwa wanashirikiana na kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha makandarasi wazawa wanashiriki katika miradi ya ujenzi kwa kuunda timu ya pamoja ya kuandaa mpango mkakati wa kuwajengea uwezo. 

Naye, Mwenyekiti mwenza kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ) Dkt. Khalid Mohamed, amesema kuwa kwa kuzingatia kazi za Serikali kwa Awamu ya Sita ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Samia Suluhu Hassan na Awamu ya Nane ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi Sekta ya Ujenzi imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwani miundombinu katika pande hizi mbili imeshamiri na hivyo kuchochea ukuaji wa utalii na hivyo kukuza uchumi wa taifa. 

“Kwa kipindi cha miaka mitatu cha Uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi kwa Zanzibar tumepata mafanikio makubwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara za Mijini na Vijijini ambapo zaidi ya kilomita 846 za barabara zinaendelea kujengwa Unguja na Pemba kwenye mtanndao wa barabara wenye takribani kilometa 1,344”, amesema Dkt. Mohamed. 

Ameongeza kuwa umuhimu wa mikutano hii ya Mashirikiano ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa kazi wanazofanya viongozi wetu wakuu hivyo ni wajibu wa wajumbe kujadili mafanikio na changamoto zinazozikabili pande zote mbili na kutafuta njia sahihi ya kuondosha changamoto hizo kwani kuimarika kwa Sekta hiyo ndio kuimarika kwa uchumi wa nchi na ustawi wa jamii. 

Awali akitoa taarifa ya Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi (SMJT), Balozi Eng. Aisha Amour, amesema kuwa mikutano ya mashirikiano ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha Muungano pamoja na kuchochea ufanisi wa utendaji wa Sekta ya Ujenzi kwa pande zote za Muungano katika kubadilishana uzoefu, utaalamu na taarifa na imewezesha kuibua fursa na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika Sekta hiyo. 

Mikutano ya Mashirikiano ni moja ya mkakati wa Serikali zote mbili kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (SJMT) na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (SMZ) katika kuunganisha Wizara na Taasisi zisizokuwa za Muungano zinazofanya majukumu yanayoshabihiana na kuwa na utaratibu wa kufanya mikutano ya mashirikiano kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji pamoja na kuibua fursa zilizopo.

Post a Comment

Previous Post Next Post