Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ameongoza mapokezi ya watalii maalum zaidi ya 150 kutoka Taifa la Marekani na baadhi ya nchi kama Uingereza ambao wamewasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) leo Novemba 4, 2023 huku wengine wakianza kufika jana kuja kufanya ziara maalum ya utalii na uwekezaji nchini.
Watalii hao ambao baadhi wanatoka taasisi kubwa za Marekani na nchi nyingine na baadhi ni wasanii kutoka Hollywood, watakuwa nchini kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo Serengeti, Ngorongoro na Zanzibar ikiwa ni sehemu tu ya ujumbe maalum wa watu wengine mashuhuri watakaofika nchini Disemba kuja kucheza pia mchezo wa Tennis ndani ya Serengeti.
Mratibu wa ziara hiyo kwa Tanzania Peter Goshen aliyesaidiana na kampuni ya Kimarekani ya Insider Expedition alisema walipata nguvu ya kuandaa ziara hiyo kubwa baada ya kuhudhuria uzinduzi wa filamu ya Royal Tour wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake walipokuwa jijini Los Angeles, Marekani April, 2022 na tangu hapo wakawa wameungana kuandaa safari hii na sasa wataleta mastaa kila mwaka.
“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alijitoa sana kufanya Royal Tour leo nifuraha kubwa kwa baadhi yetu tunapoendelea kuona urasi (legacy) ya Royal Tour inaendelea kuleta mafuriko ya watalii,” alisema Dkt. Abbasi.
Tags
Habari
