Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema katika kipindi cha miaka mitatu, uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Sh. Bilioni moja zimepelekwa Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu.
Mhe. Dkt Dugange ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chalowe wilayani humo mara baada ya kuzindua vyumba vitatu vya madarasa na matundu matatu ya vyoo yenye thamani ya Sh. Milioni 82 yaliyojengwa kupitia Mradi wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi Tanzania bara.
"Kipekee sana tunamshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake Wilaya yetu ya Wanging'ombe imenufaika sana na miradi ya elimu zaidi ya Sh Bilioni moja zimekuja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu msingi na elimu sekondari. Kwetu haya ni mafanikio makubwa sana."
"Kata hii ya Igwachanya ilikua na shule moja ya sekondari lakini ikawa inazidiwa kwa sababu idadi ya wanafunzi ni wengi. Serikali ya Rais Samia kwa kuona hilo iliamua kuleta Sh. Milioni 583 kwa ajili ya sekondari nyingine ya Mtapa, kwahiyo kata hii itakua na sekondari mbili na hivyo kumaliza changamoto ya mrundikano wa wanafunzi kwenye sekondari ya awali," amesema.
Amesema Shule ya Msingi Chalowe ilikuwa na changamoto ya madarasa kutokana na yaliyokuwepo awali kuwa chakavu lakini kukamilika kwa vyumba hivyo vitatu kutasaidia kuondoa changamoto iliyokuwepo na kusisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kumaliza kero ya miundombinu ya elimu.
