
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa mradi wa maji wa Lugenge mkoani Njombe, ambao umefikia asilimia 82 ya ujenzi unaogharimu shilingi bilioni 8.7 na kutarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi elfu kumi.
Mhe. Dkt. Mpango amewahakikishia wananchi wa eneo la Ramadhani kuwa Serikali itaendelea kuwaletea maendeleo na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwapatia wananchi majisafi, salama na yenye kutosheleza kwa asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.

Ameielekeza Wizara ya Maji kukamilisha mradi wa maji wa Lugenge kama ulivyopangwa kwa kuwa fedha zipo na kufanyia kazi suala la kuwalipa fidia wananchi waliopisha maeneo ya miradi ya maji.
Kwa upande wake ,Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutenga fedha kiasi cha shilingi Bilioni 8.7 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa chanzo cha Lugenge mkoani Njombe, na amewaahidi wananchi mradi huo utakamilika kwa wakati ifikapo mapema mwezi Februari, 2024.