KAMATI YA TAMISEMI YARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA MIRADI YA ELIMU- SINGIDA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhishwa na hatua iliyofikia ya ujenzi wa  shule mpya kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na mradi wa kuboresha elimu ya Awali na Msingi (BOOST).

Kauli hiyo imetolewa  Oktoba 27, 2023  wakati wa ziara ya kikazi ya  kamati hiyo katika Mkoa wa Singida  ya kukagua miradi ya elimu  inayotekelezwa kupitia mradi wa SEQUIP na BOOST.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Justin Nyamoga(Mb) amesema, wakiwa ni  wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanafarijika kuona  fedha zinazopitishwa na bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa na kwa kuzingatiwa thamani ya fedha iliyotewa.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Mhe. Nyamoga ameupongeza uongozi wa   Mkoa wa Singida kwa usimamizi mzuri wa fedha kiasi cha shilingi  milioni  544 kwa ajili ya  ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Nkuhimtaturu ilipo kata ya Ikungi  Halmashauri  ya Ikungi na ujenzi wake kufikia asilimia 95.

Amesema, kukamilika kwa shule hiyo ni dhahiri kuwa itasaidia kupunguza changamoto nyingi ikiwemo umbali wa kutembea muda mrefu kwa watoto lakini pia itapunguza kukaa kwa mrundikano kwa wanafunzi  madarasani. 

" Kwa niaba ya kamati hii, tunamshukuru sana  Rais Mhe. Dkt. Samia Suluh Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu kwa maslahi ya nchi yetu" Mhe. Nyamoga

Kwa upande wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi Imbele iliyojengwa kupitia mradi BOOST iliyogharimu shilingi mil. 493 iliopo Halmashauri ya Manispaa ya Singida  Mhe. Nyamoga amesema, kipindi cha zamani  ilikuwa kila mzazi anataka kumpeleka mtoto wake shule za kulipia(private) kutoka na mazingira lakini  sasa uwepo wa mazingira mazuri katika shule zetu za Serikali  wazazi wengi wanapeleka watoto katika shule za Serikali  hivyo, ni  jukumu letu kwa pamoja kama  wazazi kuhimiza watoto wetu kwenda shule kusoma lakini pia kuwa walinzi na kuitunza miundombinu ya shule  ambayo Serikali imetumia gharama kubwa kuijenga.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde  ameishukuru Kamati hiyo na kuiahidi yale yote walioyaelekeza na kutoa ushauri wataendelea kuyafanyia kazi na kuieleza kamati hiyo kuwa, taswira walioiona kwa miradi ya elimu katika Halmashauri ya Ikungi na Manispaa ya Singida.

Amesema kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na Elimu ya Msingi (BOOST )Serikali  inaendelea kujenga shule nyengine mpya katika Halmashauri zote 184.

Naye Afisa Elimu Mkoa Singida Dkt. Elpidius Baganda amesema katika mwaka wa fedha  2022/23  Mkoa wa Singida  ulipokea fedha kutoka mradi wa BOOST kwa ajili ya ununuzi wa  samani na ujenzi wa shule mpya 12 za msingi na kwa upande wa mradi wa SEQUIP  tsh.bil 6.3 zilipokelewa  kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wasichana ya sayansi na shule mpya 8 za  sekondari za kata. 

Aidha, Kamati ya TAMISEMI imeutaka uongozi wa Mkoa wa Singida kushirikiana na Mamlaka ya Maji Singida, Tanesco na TARURA kushugulikia changamoto za za kukosekana kwa huduma ya maji, umeme na barabara  katika shule ya sekondari mpya iliyojengwa Ikungi na kuhakikisha huduma hizo zinafika   kabla ya wanafunzi kufungua shule Januari, mwakani.

Post a Comment

Previous Post Next Post