WANANCHI KATA YA IPAGALA WAPONGEZA UJENZI WA SHULE YA MSINGI SWASWA



Wananchi wa Kata ya Ipagala Jijini Dodoma wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa ujenzi wa Shule ya Msingi Swaswa  ambayo imekuwa ni hitaji kubwa la wananchi hao kwa miaka mingi kwakuwa wanafunzi wa maeneo hayo wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata shule.


Pongezi hizo zilitolewa wakati wa Mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde katika kata ya Ipagala viwanja vya Shule ya Msingi Swaswa.


Akiwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Diwani wa Kata ya Ipagala Mh. Gombo Kamuli Dotto amesema ujenzi wa Shule ya Msingi Swaswa ni ukombozi mkubwa kwa wanafunzi wa kata ya Ipagala eneo la Swaswa ambao walikuwa wanatembea umbali mrefu,na kutumia fursa hiyo kumshukuru Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan na Mbunge Mh. Anthony Mavunde kwa ushirikiano mkubwa unaopelekea kutekelezwa kwa miradi ya ujenzi wa kituo cha Afya,Nyumba za walimu,barabara,visima vya maji na zoezi la upimaji kwa maeneo yote ya mitaa yaliyobaki.


Akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita imejipanga kwa dhati kabisa katika kuboresha na kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi na kwamba ndani ya miezi mitatu zimejengwa Shule za Msingi 5 katika Jiji la Dodoma ikiwemo Shule ya Msingi Swaswa.


“Mtakumbuka kwamba mwaka 2020 mimi na Diwani Gombo tulikuja hapa kuahidi ujenzi wa Shule ya Msingi Swaswa na leo nina furaha kubwa kuiona ahadi hii imetekelezeka na kuwapunguzia mwendo mrefu watoto wa shule.


Tunaishukuru serikali chini ya Mh.Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa ujenzi wa shule hii ambayo ni mkombozi mkubwa kwa wanafunzi wa eneo la Swaswa”Alisema Mavunde


Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde. Charles Mamba na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Alhaj Jabir Shekimweri wamepongeza kasi kubwa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali na kutaka viongozi wote waendelee kushirikiana kwa pamoja katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Post a Comment

Previous Post Next Post