Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Deogratius Ndejembi amewataka Maafisa Ugani nchini kuifanyia kazi agenda ya 10/30 na takwimu za kilimo ili kuwainua wakulima nchini.
Mheshimiwa Ndejembi ameyasema hayo wakati akikagua na kujionea shughuli za Taasisi mbalimbali kwenye maonesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Kati Dodoma na kusema kuwa Wizara yenye dhamana na masuala ya Kilimo inapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na Wagani waliopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kutimiza malengo yake.
“sisi ndio wapiganaji wa Wizara ya kilimo, sisi na Wagani wetu (Maafisa Kilimo) ndio wachangamshaji wa kilimo nchini kwani ndio tunawafikia wakulima kule chini walipo, tuache kufanya kazi kwa mazoea ili tufikia malengo ya Serikali ya kuboresha kilimo” amesema Mhe. Ndejembi.
Aidha, Ndejembi amewaagiza Maafisa hao kutumia takwimu za kilimo ambazo zitasaidia kujua matokeo na mwelekeo wa sura ya kilimo nchini kwa kila mwaka ili kutoa tathmini na tafiti za kweli bila kufanya makadiria ya takwimu za kilimo kwani hazina tija kwa wakulima na Taifa lakini wao pia watashindwa kuwashauri vizuri wakulima ikiwa ni pamoja na kushindwa kutimiza agenda ya 10/30 Mpango wa Serikali chini ya Wizara ya Kilimo unaolenga kuwainua wakulima na kukiinua kilimo nchini Tanzania ili kufikia lengo la kukuza Sekta ya Kilimo kwa 10%
Amesema kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI agenda kubwa ni kuisaidia Wizara ya Kilimo kwa kuwa tusipofanya kazi vizuri tunawaangusha katika utendaji wao na hivyo kila mtu hana budi kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Katika hatua nyingine Mhe. Ndejembi amekagua vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu waliopata mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri kuzifanyia biashara zenye manufaa na hatimaye kuirejesha mikopo hiyo ili vikundi vingine vinufaike na mikopo ya Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini badala ya kuchukulia kama ni fedha za msaada kutoka Serikalini.
Awali akikagua mabanda mbalimbali alitembelea banda la Ofisi ya Rais TAMISEMI na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwani ndiyo Wizara yenye dhamana na Watanzania kwa kiasi kikubwa.
Kauli Mbiu ya Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu ni “Vijana na wanawake ni Msingi imara wa Mifumo Endelevu ya hakula”
