Wananchi wa Mtaa wa Chinyoyo,Kata ya Kilimani Jijini Dodoma wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde kwa ujenzi wa Shule ya Msingi mpya ya Chinyoyo ambayo itasaidia kuwapunguzia umbali mrefu wa kutembea kufuata shule na hivyo sasa watoto wa mtaa huo watasoma katika eneo lao.
Akitoa maelezo ya awali Diwani wa Kata ya Kilimani Mh. Neema Mwaluko amesema kwamba wanafunzi wengi wanaotoka eneo hili la Chinyoyo wanatembea umbali mrefu kufuata shule katika kata za jirani na hivyo kutembea umbali mrefu ambapo imekuwa ni kero kubwa kwa watoto hasa wa kike ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali wakiwa njiani.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye ndio alizindua zoezi la uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa madarasa hayo ameeleza yafuatayo;
Eneo hili limekuwa na changamoto ya kuwa na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo shule,hii ni kutokana na historia ya eneo hili ambapo palitengwa kuwa ukanda wa kijani kwa ramani ya 1976 kabla hapajabadilishwa matumizi na kuwa sehemu ya makazi miaka ya hivi karibuni na kumalizika kwa mgogoro wa ardhi wa muda mrefu.
Nilikuja hapa miezi kadhaa iliyopita mwaka huu na nikawaahidi wananchi kwamba tutaanza ujenzi wa shule ndani ya mwezi Julai,2023.
Leo nimefurahi ahadi imetimia na tumeanza kuchimba msingi kwa kushirikiana na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne (4) ya hatua ya awali ambapo jumla ya Tsh 80,000,000 zimetolewa na serikali chini ya uongozi wa Mh.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan
Ofisi ya Mbunge pia itajenga darasa moja katika kuunga mkono jitihada hizi za serikali na wananchi ili kuboresha elimu katika mtaa wa Chinyoyo.
Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa CCM Kata ya Kilimani,Katibu wa CCM Kata Ndg. Lotary Ndimbo amepongeza jitihada za serikali na viongozi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM 2020-2025 na kutaka ujenzi huo usimamiwe vizuri ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi.