WAKURUGENZI WAPYA WATAKIWA KUSIMAMIA MAPATO ILI HALMASHAURI ZIJITEGEMEE KIBAJETI


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru amewataka Wakurugenzi wapya wa Halmashahuri,  kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili Mamlaka hizo zijitegemee kiuchumi.

Bw. Ndunguru ametoa rai  hiyo Jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo kwa Wakurugenzi hao wapya 16 walioteuliwa hivi karibuni na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Bw.  Ndunguru amewataka kushiriki kikamilifu kwenye mafunzo hayo ya siku mbili ili waweze kukabiliana na changamoto za kiutendaji, kutimiza malengo ya Halmashauri, kujifunza majukumu, maadili, kupambana na rushwa, kusimamia miradi, hoja za CAG, mawasiliano ya Serikali, uzoefu wa wenzao, kujitegemea kiuchumi na kuwajibika ipasavyo kazini.

“Ili tuweze kujitegemea kibajeti, tunategemea zaidi uwezo wetu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Hakikisheni mnasimamia kikamilifu ukusanyaji huo, fedha zote zinafikishwa benki kwa mujibu wa taratibu, na mifumo ya kielektroniki pamoja na mashine za PoS (mashine za kukusanyia mapato) zinatumika katika kila chanzo,” amesisitiza Katibu Mkuu Bw. Ndunguru.

Aidha, amewataka kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuhakikisha fedha za mapato ya ndani zilizotengwa kwa ajili ya miradi zinatumika kwenye miradi hiyo, na kuchukua hatua stahiki kuhusu mapendekezo ya CAG. Amewataka pia Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na watumishi kuandaa mipango kazi, kuwajibika kwa wananchi, kutatua kero zao hadi mwisho, na kujenga mahusiano mazuri ya kikazi na Waheshimiwa Madiwani.

Bw. Ndunguru amehitimisha kwa kuwataka Wakurugenzi hao kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi na kuepuka kuzalisha madeni yasiyo ya lazima. Amesema anatarajia mafunzo hayo yatawajengea umahiri, uwajibikaji na kujiamini katika kusimamia mipango ya Halmashauri zao, kwa manufaa ya wananchi na utoaji bora wa huduma.

Naye Bw. Charles Mwaitege, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi  amesema kupitia mafunzo hayo yanawaandaa ili kujua ni jinsi gani wanaweza kukusanya na kutunza mapato kwa kuzuia mianya ya upotevu wa mapato na kushirikiana na watumishi kuunda timu za ufuatiliaji za Serikali kwa kutumia mifumo ya POS ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za mapato  ya Serikali.

Mafunzo kwa Wakurugenzi wapya wa Halmashauri yanafanyika chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI,  lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kusimamia Halmashauri zao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post