GHANA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA KATIKA KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO



Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ametoa wito kwa Tanzania na Ghana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo kushiriki kikamilifu uchumi wa madini na pia katika usimamizi wa rasilimali za madini, akisisitiza kuwa wakati umefika kwa Afrika kuacha kuwa chanzo cha malighafi kwa viwanda vya nje na badala yake kutumia utajiri wake wa madini kujenga viwanda ndani ya nchi, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi wake.


Mhe. Mavunde ameyasema hayo Oktoba 21, 2026, wakati wa kikao cha pande mbili (bilateral meeting) kati yake na Waziri wa Ardhi na Maliasili wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. Emmanuel Armah-Kofi Buah, uliofanyika jijini Accra, ambapo viongozi hao wamejadili fursa za kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na maendeleo ya Sekta ya Madini kwa manufaa ya nchi hizo mbili.


Akizungumza katika kikao huo, Mhe. Mavunde amesema ni wakati muafaka sasa serikali hizi mbili zikawaangalia wachimbaji wadogo kwa jicho la uwezeshaji ule waendelee kushiriki na kuchangia kikamilifu maendeleo ya uchumi kupitia sekta ya madini.


Mavunde amesisitiza kuwa kwa muda mrefu nchi za Afrika zimekuwa zikifanya kazi kwa kujitenga katika sekta ya madini, huku rasilimali kama dhahabu, shaba, grafiti, lithiamu na madini mkakati zikisafirishwa nje ya bara hili bila kunufaisha kikamilifu uchumi wa nchi zinazozalisha madini hayo.


“Enzi ambazo Afrika inafanya kazi kama ghala la malighafi kwa mataifa mengine lazima ziishe, na lazima ziishe sasa,” amesisitiza Mhe. Mavunde, akieleza kuwa nguvu ya Tanzania na Ghana haipaswi kuishia katika uchimbaji wa madini, bali katika kuunganisha utaalamu, teknolojia utafiti na uwezo wa nchi hizo kujenga mifumo ya uzalishaji na uongezaji thamani ndani ya Afrika.


Amesema ushirikiano huo unapaswa kuelekezwa katika maeneo muhimu ikiwemo uongezaji thamani wa madini kupitia kuyeyusha, kusafisha, kuchakata, kuongeza thamani na kuzalisha bidhaa za viwandani, badala ya kutegemea mauzo ya madini ghafi na kwamba hatua hiyo itasaidia kubakiza mitaji ndani ya nchi, kukuza uwezo wa viwanda vya ndani na kutengeneza ajira zenye tija kwa vijana wa Afrika.


Katika eneo la utafiti wa kijiolojia, Mhe. Mavunde amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Ghana kubadilishana utaalamu, teknolojia na taarifa za kijiolojia ili kuimarisha uwezo wa nchi hizo kutambua rasilimali zilizopo, kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kujadiliana mikataba ya uwekezaji kwa kujiamini zaidi.


Ameeleza kuwa nchi za Afrika zinapaswa pia kuimarisha ushiriki wa wazawa katika Sekta ya Madini (Local Content) ili wananchi wasibaki kuwa wafanyakazi pekee migodini, bali waweze kushiriki kama wamiliki wa biashara, wawekezaji, wasambazaji wa bidhaa na huduma na wazalishaji wa bidhaa zinazotokana na madini.


Akizungumzia uzoefu wa Ghana, Mhe. Mavunde amepongeza hatua zilizochukuliwa na nchi hiyo katika kuwawezesha wachimbaji wadogo, akieleza kuwa Tanzania inaendelea kujifunza kutokana na uzoefu huo na kusema kuwa Tanzania pia inalenga kujifunza namna Sheria ya Madini na Tume ya Madini ya Ghana zinavyosimamia shughuli za sekta hiyo, ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa madini katika nchi hizo mbili


Kwa upande wa uwekezaji, Mhe. Mavunde amezitaka kampuni na washirika wa kimataifa kuelekeza uwekezaji wao katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini, miundombinu na shughuli za kuongeza thamani ndani ya Afrika, huku wakizingatia mikataba yenye manufaa ya haki kwa nchi mwenyeji na wananchi wake.

Aidha, amemwalika Waziri mwenzake wa Ghana pamoja na ujumbe wake kutembelea Tanzania katika miezi ijayo, kwa lengo la kuendeleza mazungumzo na kuweka mifumo rasmi ya ushirikiano, ikiwemo kuanzisha vikundi kazi vya kitaalamu vya pamoja kati ya Wizara za Madini za nchi hizo mbili.

Amesema Tanzania na Ghana zina nafasi ya kuwa mfano wa ushirikiano wa kikanda katika kubadilisha utajiri wa madini kuwa maendeleo ya viwanda na ustawi wa wananchi, hususan katika kipindi ambacho dunia inaelekea kwenye matumizi ya teknolojia na nishati safi yanayohitaji madini mkakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi na Maliasili wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. Emmanuel Armah-Kofi Buah, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano badala ya kutegemea juhudi za kila nchi pekee katika kuendeleza Sekta ya Madini, ambako amesema uzoefu wa kihistoria unaonesha kuwa utajiri wa rasilimali za Afrika haujawanufaisha kikamilifu wananchi wake kutokana na kuendelea kuuza malighafi bila kuzichakata na kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa ndani ya bara hilo.

Mhe. Buah ameeleza kuwa uongezaji thamani wa rasilimali ni msingi wa kujenga viwanda, kutengeneza ajira na kuinua maisha ya wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa Tanzania na Ghana kubadilishana uzoefu na mikakati iliyofanikiwa katika usimamizi wa Sekta ya Madini na kubainisha umuhimu wa mikataba ya madini kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazozunguka migodi, akitolea mfano wa mikataba ya maendeleo ya jamii inayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki katika matokeo ya uwekezaji wa madini.

Post a Comment

Previous Post Next Post