TARURA YAANZA UJENZI WA BARABARA YA KIBAONI–TARANGIRE, KUFUNGUA FURSA ZA UTALII NA UCHUMI MANYARA


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Manyara imeanza ujenzi wa barabara ya Kibaoni–Tarangire yenye urefu wa kilomita 6.69 ili kurahisisha usafiri na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi pamoja na kuimarisha shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

‎Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TARURA mkoa wa Manyara, Mhandisi Wilson Charles amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha safari za wananchi na wageni wanaotembelea hifadhi hiyo sambamba na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato yatokanayo na utalii.

‎Amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inaelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, hivyo kuboreshwa kwake kutarahisisha watalii kufika katika hifadhi hiyo na kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa.

‎"Barabara hii inaelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kukamilika kwake kutasaidia watalii kufika kwa urahisi zaidi na kuboresha huduma za usafiri na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa", amesema Mhandisi Wilson.

‎Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka TARURA, Mhandisi Phares Ngeleja amesema mradi huo unaendelea kusimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha  kazi zinaendelea vizuri na tunatarajia mradi huu kukamilika kwa wakati ili barabara ianze kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi na watumiaji wengine", amesema Mhandisi Ngeleja.

‎Naye, mkazi wa Kibaoni Bw. Elihuruma Yohana amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa suluhisho la changamoto za usafiri ambazo zimekuwa zikijitokeza hasa wakati wa msimu wa mvua na hivyo kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi.

‎Amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inawaunganisha wananchi na maeneo mengine huku uboreshaji wake ukitarajiwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post