TRC KUFANYA MAJARIBIO YA TRENI YA MIZIGO YA SGR (PORT LINK) KATI YA MALINDI NA PUGU, MEI 10,2026


Shirika la Reli Tanzania (TRC) linatarajia kuanza majaribio ya treni ya mizigo katika reli ya kisasa ya SGR kutoka Bandarini kupitia hadi Pugu Mei 10, 2026, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuanza rasmi kwa huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa reli hiyo kutoka na kwenda bandarini.

Hatua hiyo inafikiwa wakati kazi za mwisho za mradi huo zikiendelea kukamilishwa, ikiwemo majaribio ya mifumo ya umeme, uwekaji wa tabaka la mwisho la tuta la reli pamoja na maboresho ya miundombinu katika eneo la bandarini.

Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha kwanza cha mradi huo, Thadei Komu amesema maandalizi ya kuanza majaribio yanaendelea vizuri huku mifumo muhimu ikiwa tayari imekamilika.

Amesema kwa sasa wanaendelea na makabidhiano ya mfumo wa umeme baada ya mkandarasi kukamilisha kazi zote zinazohusu miundombinu hiyo, huku majaribio ya mfumo huo yakiendelea.

“Tunategemea kuanzia Mei 10, 2026 kuanza kupitisha treni ya mizigo kutoka Malindi hadi Pugu. Reli yenyewe imekamilika na kinachoendelea sasa ni kazi za mwisho za tabaka la tuta la reli,” amesema Komu.

Aidha amesema kuwa maboresho yanaendelea katika njia za muda mfupi za mageti ya bandarini ili kurahisisha upitishaji wa malori ya mizigo wakati shughuli rasmi za usafirishaji zitakapoanza.

Kwa mujibu wa Komu, mwisho wa mwezi huu wanatarajia kufanya operesheni ya kwanza ya upakiaji wa mizigo bandarini ambapo mizigo itapakiwa kwenye treni na kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali.

Naye Mhandisi kutoka kampuni ya Yapi Merkez, Erick Nziku amesema kazi zote kuu katika eneo la reli linaloelekea bandarini zimekamilika na kilichobaki ni hatua za mwisho za uboreshaji.

Amesema reli katika kipande chote tayari imetandikwa huku nguzo zote za umeme zikiwa zimeunganishwa na mfumo wa umeme, hali inayowezesha treni kuingia bandarini bila changamoto yoyote.

“Tumeweka mifumo ya ulinzi kwa watembea kwa miguu na magari ili kuhakikisha usalama na kuzuia ajali katika maeneo ya reli,” amesema Nziku.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka kampuni ya Yapi Merkez, Erdinc Isgoren amesema hadi kufikia mwisho wa Aprili 2026, utekelezaji wa mradi wa SGR kuelekea bandarini ulikuwa umefikia asilimia 96.6.

Isgoren amesema kazi iliyobaki kwa sasa ni shughuli ndogo ndogo za kuunganisha na kuchomea reli kuelekea bandarini baada ya utandikaji wa reli hiyo kukamilika.

“Mei 10, 2026 tutafanya majaribio ya treni kutoka bandarini hadi Pugu. Tupo tayari kwa hatua hiyo muhimu,” amesema Isgoren.

Post a Comment

Previous Post Next Post