Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar (Mb), amewasili jijini Banjul, nchini Gambia, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa African Caucus 2026 utakaofanyika kuanzia Julai 6, 2026, ukitarajiwa kuwakutanisha viongozi wa Afrika, watunga sera, wataalamu wa fedha, washirika wa maendeleo na wawakilishi wa taasisi za kifedha za kimataifa.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Banjul, Waziri Omar alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anayesimamia pia shughuli za kibalozi nchini Gambia, Mhe. Selestine Kakele.
Mkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha SDJK unatarajiwa kuwa jukwaa la nchi za Afrika kujadili masuala muhimu ya uchumi na maendeleo ya bara, pamoja na kuweka msimamo wa pamoja katika ushirikiano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia.
African Caucus ni jukwaa linalowakutanisha Magavana wa Afrika wa IMF na Benki ya Dunia kwa lengo la kuratibu msimamo wa pamoja kuhusu masuala ya usimamizi wa madeni, maendeleo ya miundombinu, mabadiliko ya tabianchi, biashara, ajira, kupunguza umasikini na mageuzi ya uchumi.
Kwa upande wa Gambia, kuandaa mkutano huo kunatajwa kuwa fursa ya kuonesha mafanikio yake katika mageuzi ya uchumi, utalii, kilimo, uwezeshaji wa vijana na maendeleo ya kidijitali, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Aidha, mkutano huo unatarajiwa kujadili changamoto zinazozikabili nchi za Afrika, ikiwemo ongezeko la madeni, uhaba wa chakula, ukosefu wa ajira na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku ukitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho zinazozingatia mazingira halisi ya bara la Afrika.
Mbali na mijadala ya kiuchumi, mkutano huo unatarajiwa kuchochea shughuli za biashara na utalii nchini Gambia kupitia ongezeko la wageni na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na taasisi za kimataifa.
