WANANCHI KONDOA MJINI WATAJWA KUWA MFANO BORA WA ULINZI WA AMANI NCHINI KWA KURIPOTI WACHOCHEZI


Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, Mariam Ditopile, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa amani, akibainisha kuwa matukio ya uharibifu wa mali, majeruhi na vifo yaliyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo yanapaswa kuwa funzo la kudumu kwa jamii kujiepusha na vurugu na chokochoko.

Akizungumza katika semina ya wenyeviti wa serikali za Mitaa, vitongoji na madiwani wa Halmashauri ya Kondoa mji, Mhe. Ditopile amesema kuwa katika baadhi ya matukio ya nyuma, vurugu zilipoanza zilisababisha madhara makubwa ikiwemo uharibifu wa mali na kupoteza maisha, hali ambayo amesema haipaswi kujirudia tena nchini.

“Tumeyaona yaliyotokea ya uharibifu wa mali, watu wamekuwa walemavu, wengine wamepoteza maisha, lakini chanzo kikubwa ni wale walioanzisha vurugu hizo,” amesema.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha uchaguzi, kulikuwa na baadhi ya chokochoko zilizoingizwa na watu kutoka nje kwa lengo la kuhamasisha mambo yasiyofaa, lakini wananchi wa Kondoa walichukua hatua kwa haraka kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Amesema hatua hiyo ilisaidia kudhibiti hali mapema na kuhakikisha wilaya ya Kondoa inabaki salama, huku akivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanyia kazi taarifa za wananchi bila kupuuza.

“Wananchi wenyewe walilinda amani yao. Tunawapongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuchukua hatua kwa wakati, Kondoa ikaendelea kuwa salama,” amesema.

Mhe. Ditopile ameongeza kuwa wananchi wakipewa nafasi na kuhamasishwa kuwa sehemu ya ulinzi wa amani, kazi ya vyombo vya dola inakuwa nyepesi na taifa linapata utulivu wa kudumu.

Aidha, amewataka wananchi kujiepusha na ushiriki katika matukio ya uvunjifu wa amani, hususan katika matukio ya kijamii kama Sabasaba, akisisitiza kuwa wanapaswa kushiriki shughuli hizo kwa amani na utulivu.

“Tuwaambie wananchi wetu kuwa nchi iko salama. Wanaweza kwenda kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba kutembelea mabanda na kufanya shughuli zao kwa amani bila kuvunja sheria,” amesema.

Amehitimisha kwa kuwataka wananchi kumtukuza Mungu, kuheshimu mamlaka zilizowekwa, na kufuata maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama ili kuendelea kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post