NAIBU KAMISHNA IDARA YA UPELELEZI WA KODI AWAPATIA ELIMU WATUMISHI WAPYA WA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA


Naibu Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Kodi, Bi. Felisiana Nkane, amekutana na watumishi wapya wa TRA ambao wapo kwenye mafunzo elekezi Chuo cha Kodi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapatia uelewa kuhusu majukumu ya Idara ya Upelelezi wa Kodi, mbinu za kipelelezi pamoja na taratibu zinazotumika kubaini na kudhibiti ukwepaji wa kodi. Akizungumza na watumishi hao, amesema Idara hiyo ina jukumu la kulinda mapato ya Serikali kwa kupambana na wahalifu wa kiuchumi, hususani ukwepaji kodi, kupitia ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia.

Vilevile, Bi. Nkane amesema elimu hiyo itawasaidia waajiriwa hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi watakapopangiwa vituo vya kazi, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za Idara kuanzia ukusanyaji wa taarifa, uchakataji wake hadi kufanikisha uchunguzi. Aidha, amewakumbusha kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kujituma na kufanya kazi kwa uadilifu, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo chachu ya mafanikio na kufikia malengo ya Mamlaka.

Pia amesisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa karibu na wadau na watoa taarifa, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya ukwepaji wa kodi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post