WAZIRI KAIRUKI APIGA KURA YA NDIYO, BUNGE LAPITISHA BAJETI KUU YA SERIKALI KWA MWAKA 2026/27


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Angellah Kairuki, leo ameshiriki Mkutano wa Tatu wa Bunge, Kikao cha Hamsini na Tano, jijini Dodoma, ambapo amepiga kura ya ndiyo kuunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Katika hatua hiyo muhimu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali yenye thamani ya Shilingi trilioni 62.33 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Bajeti hiyo imekusudiwa kuendeleza juhudi za Serikali katika kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati, na kuboresha utoaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

Aidha, bajeti hiyo imeweka msisitizo katika kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utoaji wa huduma za umma na kuchochea maendeleo ya taifa, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatoa mwelekeo wa utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku ikitarajiwa kuchangia katika ujenzi wa uchumi imara, shindani na jumuishi unaowanufaisha Watanzania wote.

Post a Comment

Previous Post Next Post