TAGCO YASISITIZA WANAMAWASILIANO WA SERIKALI KUWA WASHIRIKA WA KIMKAKATI WA MAENDELEO


Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) kimesema nafasi ya mwanamawasiliano wa Serikali imekua na sasa inahitaji wataalamu hao kuwa washirika wa kimkakati katika utekelezaji wa agenda za maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka na Kongamano la Wanamawasiliano wa Serikali 2026 jijini Mwanza, Mwenyekiti wa TAGCO, Karim Meshack amesema zama za mwanamawasiliano kuishia kuandika taarifa kwa vyombo vya habari pekee zimepitwa na wakati.

Amesema mwanamawasiliano wa Serikali wa sasa anapaswa kuwa mfasiri wa sera, mshauri wa kimkakati wa taasisi, mjenzi wa uelewa wa umma na daraja linalounganisha Serikali na wananchi.

“Tunawajibika kusaidia wananchi kuelewa Serikali inafanya nini, kwa nini inafanya, changamoto zilizopo na namna hatua zinazochukuliwa zinavyochangia maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla,” alisema Meshack.

Alibainisha kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mawasiliano yaliyoratibiwa, yenye ushahidi na yanayowafikia wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

Kwa mujibu wa Meshack, kongamano hilo linatoa fursa kwa wanamawasiliano wa Serikali kujadili mbinu za kuwasilisha kwa ufanisi nguzo na vichocheo vya Dira 2050 kwa umma, huku likiimarisha mshikamano na weledi ndani ya taaluma hiyo.

Mkutano huo umehudhuriwa na wanamawasiliano wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini pamoja na wadau wa sekta ya habari na mawasiliano.

Post a Comment

Previous Post Next Post