SAMIA AITAKA BOT KUJENGA UCHUMI UNAOGUSA MWANANCHI, AWATAKA WAFANYABIASHARA WADOGO KUPATIWA MIKOPO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuimarisha uwezo wake wa kutambua mapema mwelekeo wa uchumi na kukabiliana na athari za misukosuko ya kimataifa inayotikisa uchumi wa dunia.

Akizungumza leo, Dkt. Samia amesema mafanikio ya mageuzi ya kiuchumi hayapaswi kubaki kwenye takwimu za ripoti pekee, bali yanapaswa kutafsiriwa katika kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida kupitia upatikanaji wa mitaji, ajira na fursa za kiuchumi.

Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa taasisi za fedha kuwawezesha wanawake na vijana kupata mikopo hata kama hawana dhamana za kawaida kama nyumba au magari, akibainisha kuwa uaminifu, historia ya biashara na miamala vinaweza kutumika kama vigezo vya kuwapatia mikopo.

Aidha, amesema mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kutoka asilimia 6.6 ya pato la taifa mwaka 1994 hadi takriban asilimia 16 mwaka jana, jambo linaloonyesha nchi ipo katika mwelekeo sahihi wa kukuza uchumi.

Kwa upande mwingine, amezitaka taasisi za fedha kuongeza uwazi katika utoaji wa mikopo kwa kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu gharama na masharti ya mikopo kabla ya kufanya maamuzi.

Rais Samia amesema kuanzia Julai 1, 2026 Tanzania itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye thamani ya dola trilioni 1 pamoja na kuongeza kipato cha wastani hadi dola 7,000 kwa mtu.

Post a Comment

Previous Post Next Post