Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mambi lililojengwa katika barabara ya Chiwindi - Mtimbwilimbwi lenye urefu wa mita 13 limeleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa kata za Mtimbwilimbwi, Njengwa na Hinju katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Mtwara Mhandisi Khatibu Nunu wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa barabara wilayani humo na kubainisha kuwa ujenzi huo umetekelezwa kupitia Mradi wa RISE, programu ya kuondoa vikwazo vya barabara (Bottleneck).
Amesema changamoto walizokuwa wanazipata wananchi wa eneo hilo hasa kutoka kijiji cha Majengo, Mtimbwilimbwi, Njengwa na Hinju ni kujaa kwa mto Mambi hivyo kukwamisha wananchi hao kuzifikia huduma za kiuchumi na kijamii upande wa pili.
Mhandisi Nunu amezitaja huduma hizo ni pamoja na usafirishaji wa mazao ya kilimo kama vile korosho na Ufuta kwa kuyatoa kutoka mashambani na kuyapeleka maeneo ya maghala kwenye Vyama vya Msingi, huduma za afya na shule pamoja na huduma za kiutawala ambazo zote zinapatikana upande wa pili mjini Nanyamba.
"Ujenzi wa daraja hili kwa upande mwingine limewawezesha wananchi wa maeneo haya kufika barabara kuu ya Mtwara - Nanyamba - Tandahimba. Kwa hiyo wakipita hapa kwenye daraja ni kiunganishi muhimu katika eneo letu la Nanyamba kata ya Mtimbwilimbwi." amesema.
Naye Bi. Amina Ally Ayandike, mkazi wa kata ya Mtimbwilimbwi amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa huduma hiyo aliyowapatia wananchi wa Mtimbwilimbwi kwa sababu walikuwa na mkwamo mkubwa katika barabara za mashambani hasa kipindi cha masika.
"Sasa hivi hakuna mtu anashindwa kwenda shambami eti kwa sababu maji yametuzuia hapana. Hapo awali tulikuwa tukienda mashambani tunarudia njiani kwa sababu ya mto kujaa maji. Tunamshukuru sana. " amefafanua Bi. Amina.
Kwa upande wake Bw. Juma Mohamed Henda amesema gharama za usafirishaji kabla ya ujenzi wa daraja hilo ilikuwa juu kwa sababu ya mzunguko huku akitolea mfano wa kukodi boda boda kutoka Kijiji cha Mtimbwilimbwi hadi makao makuu ya Halmashauri hiyo Nanyamba ilikuwa shilingi 15,000 na gari ilikuwa kati ya shilingi 40,000 hadi 45,000 lakini sasa hivi ni shilingi 5000 tu.
