Migogoro ya Wakulima na Wafugaji ni sumu inayoweza kuvunja amani isipotatuliwa mapema. Wananchi wako tayali kumaliza migogoro ila tu inasisitizwa kwa viongozi pawepo na ushirikishwaji wa pamoja kwa pande zote kupitia mikutano ya vijiji na vikao vya pamoja wakati wa utatuzi wa migogoro.
Afisa Tarafa ya Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku leo Jumatano Juni 17, 2026 ameongozana na viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Bundaza kwenye Kata ya Nyakibimbili pamoja na Afisa Kilimo na Mifugo wa Kata hiyo kusikiliza wananchi wa Kitongoji cha Kishenge wanaolima na kufuga katika eneo la Kilebe na kumaliza misuguano kati ya Wakulima na Wafugaji wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo hilo la Kilebe.
Kwenye kusikiliza kero hiyo kati ya Wakulima na Wafugaji na kusuluhisha, Bwanku aliongozana na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Ndugu, Charles John, Mtendaji wa Kijiji Bi. Wivina Anatory, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Ndugu Respicius Bitegeko, Afisa Kilimo wa Kata, Eng Syliakus Kagyabukama, Afisa Mifugo Ndugu Benetson Balayangaki pamoja na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji.
Afisa Tarafa Bwanku aliwaongoza viongozi wenzake kusikiliza kila hoja zote za wananchi kwa pande zote mbili za Wakulima na Wafugaji na kukubaliana kuweka utaratibu wa kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kulima na kufuga kwenye eneo hilo la Kijiji huku utaratibu mzima ukiwa shirikishi kuhusisha pande zote mbili kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji utakaohusisha wananchi wote.
Viongozi wote walisisitiza wananchi suala la amani na ujirani mwema kwa kuhakikisha kila mmoja anafanya shughuli zake kwa kufuata utaratibu bila kujaribu kuvunja amani.
