Wizara ya Afya imesema ipo katika majadiliano na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhusu mpango wa kuanzisha behewa maalum la ambulance ndani ya treni za reli ya kisasa ya SGR ili kutoa huduma za afya kwa abiria wanapokuwa safarini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa #NusuMudaKoteKote yenye lengo la kuadhimisha miaka miwili tangu kuanzishwa kwa huduma ya SGR Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema mpango huo unalenga kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa haraka ndani ya treni, hasa kwa wagonjwa wa dharura na abiria wenye uhitaji wa huduma mbalimbali za kitabibu.
Amesema kutokana na ongezeko la matumizi ya usafiri wa SGR kwa makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo viongozi wa serikali, wafanyabiashara na wagonjwa, serikali imeona umuhimu wa kuwepo kwa huduma hizo ndani ya treni.
“Mjadala wetu na Mkurugenzi Mkuu wa TRC unaendelea vizuri na tunaamini kwamba kila treni itakayotoka Dar es Salaam kwenda Dodoma itakuwa na behewa maalum la ambulance kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za afya,” alisema Mchengerwa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, huduma zitakazotolewa ndani ya behewa hilo ni pamoja na upimaji wa moyo, uzito, shinikizo la damu pamoja na huduma za kwanza kwa wagonjwa wa dharura watakaojitokeza wakati wa safari.
Ameongeza kuwa serikali imeamua kuja na mpango huo ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu hata wanapokuwa safarini kupitia reli ya kisasa ya SGR.
