UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA UNAONESHA DHAMIRA YA KWELI YA RAIS SAMIA - MBUNGE ASHA FERUZI


Mbunge wa Viti Maalum kundi la vyuo na vyuo vikuu, Asha Feruzi amesema bajeti ya Wizara ya Afya inaonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya bungeni, Feruzi amesema serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu ya tiba pamoja na kuongeza watumishi wa afya nchini.

Amesema tangu mwaka 2021 hadi 2026, serikali imefanikiwa kujenga vituo vipya vya afya 3,530 ambavyo havikuwepo hapo awali, zahanati 403 pamoja na hospitali 71 zikiwemo hospitali za mikoa ya Katavi, Njombe, Geita, Simiyu na Songwe.

Mhe. Feruzi amesema ndani ya siku 100 tangu kuapishwa kwa Rais Samia, serikali ilitoa kibali cha kuajiri watumishi wa kada ya afya 5,000 kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na ustawi wa afya.

Aidha amesema wananchi wengi hupata huduma za afya katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo karibu na maeneo yao, hivyo ameiiomba Wizara ya Afya kuendelea kuboresha na kuongeza vituo hivyo katika kata mbalimbali nchini.

Kuhusu bima ya afya kwa wote, Feruzi amesema mpango huo utasaidia wananchi wengi wanaopata huduma katika zahanati na vituo vya afya, hivyo kuna umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi pamoja na huduma za afya ya msingi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.

Pia amesema licha ya sera kuelekeza watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na wazee kupata huduma za afya bila malipo, bado kuna baadhi ya maeneo wananchi wanatozwa fedha kinyume na utaratibu, jambo ambalo linahitaji usimamizi wa karibu.

Katika hatua nyingine, ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuboresha mifumo ya kidijitali inayowezesha hospitali kusomana taarifa za wagonjwa, akisema hapo awali wagonjwa waliokuwa wakipewa rufaa walilazimika kuanza upya vipimo walipofika hospitali za rufaa jambo lililokuwa likiongeza gharama na usumbufu kwa wananchi.

Amesema kwa sasa mifumo hiyo inasomana kwa zaidi ya asilimia 90 katika hospitali za rufaa, hatua ambayo imeongeza ufanisi wa utoaji huduma za afya nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post