Serikali imeweka mkakati wa kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034 unaolenga kuimarisha miundombinu na mifumo ya TEHAMA ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Kairuki, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo amesisitiza kuwa, mkakati huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa 2025 na unalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za mawasiliano na teknolojia ya habari.
Kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Serikali imeboresha mifumo ya mawasiliano na kuandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mkakati, ambao utawezesha Serikali na sekta binafsi kutoa taarifa za hatua zilizofikiwa kwa kila kiashiria.
Hatua hii inalenga kuhakikisha TEHAMA inachangia kwa usahihi katika Pato la Taifa na kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi za umma na sekta binafsi imeanza kukusanya takwimu za uchumi wa kidijitali kupitia Akaunti ya Upimaji wa Uchumi wa Kidijitali (DESA), ili kuongeza wigo wa kupima mchango wa sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari katika uchumi wa taifa.
Waziri Kairuki ameeleza kuwa, mikakati hii ni hatua ya kitaifa inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi imara wa kidijitali, unaowezesha wananchi wote kufikiwa na huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari, sambamba na kuimarisha nafasi ya taifa katika teknolojia ya kisasa barani Afrika.
