TAHADHARI YA EBOLA YATOLEWA NCHINI – SERIKALI YAIMARISHA UCHUNGUZI MIPAKANI


Serikali imeweka tahadhari ya juu kufuatia taarifa za mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ulioripotiwa katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda, huku Shirika la Afya Duniani likitangaza hali hiyo kuwa dharura ya kiafya ya kimataifa.

Akitoa taarifa kwa umma, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace E. Magembe amesema Tanzania bado iko salama na hakuna kisa chochote kilichothibitishwa cha Ebola nchini hadi sasa.

Hata hivyo, kutokana na mwingiliano mkubwa wa kijamii na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi zilizoathirika, Serikali imeongeza kasi ya hatua za kinga na ufuatiliaji ili kuzuia maambukizi kuingia nchini.

Dkt. Magembe ameeleza kuwa Ebola husababishwa na virusi vinavyotoka kwa wanyama kama popo na sokwe, na huenea kati ya binadamu kupitia kugusa majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au vitu vilivyoguswa na mgonjwa, ikiwemo pia miili ya marehemu.

Amesema dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa, uchovu, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa, kutapika na kuharisha, huku katika hatua kali wagonjwa wakionyesha kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili.

Serikali imesema tayari imechukua hatua kadhaa za dharura ikiwemo kuimarisha uchunguzi kwa wasafiri mipakani, bandari na viwanja vya ndege, kuongeza utayari wa vituo vya afya, na kupeleka timu za wataalamu katika maeneo hatarishi.

Hatua nyingine ni kuimarisha elimu kwa umma, uratibu na nchi jirani, kuandaa vituo maalum vya huduma kwa wagonjwa endapo maambukizi yatajitokeza, pamoja na kuhuisha mwongozo wa wasafiri kuanzia Mei 19, 2026.

Serikali pia imetoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi wa mikono, kuepuka kugusa majimaji ya mwili wa wagonjwa au marehemu, kuepuka ulaji wa mizoga ya wanyama, na kuwahi vituo vya afya pindi dalili zinapojitokeza.

Wananchi wametakiwa kuripoti matukio yanayohusiana na dalili za Ebola kupitia namba 199 bila malipo, na kuendelea kufuata taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka za serikali pekee.

Serikali imesisitiza kuwa hatua zote za tahadhari zinaendelea kuchukuliwa ili kuzuia mlipuko wowote wa ugonjwa huo nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post