Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa Waandishi Waendesha Ofisi katika kusaidia viongozi na watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Dkt. Nchimbi amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Kitaaluma wa Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) unaofanyika katika Ukumbi wa Ngurdoto mkoani Arusha.
Amesema waandishi waendesha ofisi ni sehemu muhimu ya taasisi wanazofanyia kazi kwa kuwa ndiyo sura ya kwanza ya huduma kwa wananchi wanaofika katika ofisi mbalimbali.
Aidha, amewataka kuendelea kuwa wakarimu, wenye heshima na kutunza siri za kazi huku wakitekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu.
Makamu wa Rais pia amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kuendelea kuimarisha taaluma hiyo hadi kufikia ngazi ya shahada ya uzamili, hatua iliyowawezesha waandishi waendesha ofisi kushiriki katika maamuzi ya kisera na upangaji wa mikakati.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali itaendelea kushirikiana na TAPSEA katika kuboresha maslahi, mafunzo na maendeleo ya kitaaluma ya wanachama wake.
Naye Mwenyekiti wa TAPSEA, Bi. Zuhura Maganga amesema taasisi hiyo imeendelea kupata mafanikio katika kukuza taaluma ya uandishi na uendesha ofisi kupitia kuanzishwa kwa programu mbalimbali za elimu ya juu nchini.
