Wanawake nane kutoka sekta mbalimbali wametunukiwa Tuzo za Malkia wa Nguvu Kanda ya Kaskazini katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa AICC, Jijini Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Mkurugenzi wa Utalii Tanzania, Thereza Mugobi amesema kuwa maadhimisho ya miaka 10 ya Jukwaa la Malkia wa Nguvu yameendelea kuwa chanzo cha matumaini, fursa na uwezeshaji kwa wanawake nchini.
Amesema jukwaa hilo limekuwa likifungua milango kwa wanawake wengi kuonesha uwezo wao katika jamii na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia sekta mbalimbali.
“Ninaamini mwanamke akipewa nafasi habadilishi maisha yake pekee, bali hubadilisha familia na jamii kwa ujumla,” amesema kupitia salamu za Waziri Dkt. Kijaji.
Washindi waliotunukiwa tuzo hizo ni:
Leah Pantaleo Asenga – Sekta ya Huduma na Chakula
Dativa Koyanga – Sekta ya Kilimo Biashara
MWEDO (Maasai Women Development Organization) – Sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii
Mariam Chuma Kobelo – Utumishi Bora Sekta ya Umma
Miriam Oscar Kaaya – Sekta ya Elimu, Malezi na Ulinzi wa Mtoto
Christine Mwakatobe – Sekta ya Diplomasia ya Uchumi na Utalii
Carolyn Kandusi – Sekta ya Mapinduzi ya Kidigitali na Maendeleo ya Jamii
Mary Msonsa – Sekta ya Biashara, Uvumbuzi na Ajira
Jukwaa la Malkia wa Nguvu linaendelea kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, likilenga kuibua na kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini. Kwa mwaka huu, shughuli hizo zimeanza Kanda ya Kati kabla ya kuendelea Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine nchini.
