Balozi Maulidah Hassan, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, leo amewasilisha nakala za Hati zake za Utambulisho kwa Mheshimiwa Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Usultani wa Oman.
Hatua hii muhimu inaashiria kuanza rasmi kwa majukumu yake kama Balozi wa Tanzania nchini Oman ambapo ataenda kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliokuwepo, urithi wa pamoja na urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili.
Katika mazungumzo yaliyofanyika, Balozi Maulidah Hassan alisisitiza kuwa dhamira yake itaongozwa na misingi ya 3Rs: Kupitia upya (Review), Kufufua (Revive), na Kuchochea upya (Revitalize) ushirikiano kati ya Oman na Tanzania.
Msisitizo mkuu utakuwa ni kuunda fursa za pamoja za kiuchumi kwa kuoanisha Dira ya Oman 2040 na Dira ya Tanzania 2050, ili kubadilisha historia yao ya pamoja kuwa maendeleo yanayoonekana na yanayonufaisha wananchi wa nchi zote mbili.
Aidha, Balozi Maulidah Hassan amepongeza mchango mkubwa wa kidiplomasia wa Oman katika juhudi za amani Mashariki ya Kati, na kusisitiza uungaji mkono wa Tanzania katika kuleta amani na utulivu duniani.
Balozi Maulidah, ametoa pia shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata wakati wa kuwasilisha nakala za Hati na ameahidi kufanya kazi kwa ukaribu ili kuimarisha na kukuza ushirikiano wa nchi mbili.
